Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

MKURUGENZI KADUSHI AWATAKA MAKATIBU SHERIA KUTUMIA VIZURI MFUMO NA KUWA WAALIMU KWA WENGINE.
05 Jan, 2022
MKURUGENZI KADUSHI AWATAKA MAKATIBU SHERIA KUTUMIA VIZURI MFUMO NA KUWA WAALIMU KWA WENGINE.


Mkurugenzi Divisheni ya Utaifishaji mali, Makosa yanayovuka mipaka na kupangwa kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma Bw. Paul Kadushi amewataka Makatibu Sheria na baadhi ya Mawakili wa Serikali kwenda kuwa waalimu wazuri wa kufundisha jinsi ya kutumia mfumo katika kufanya kazi za Taasisi kwa watumishi wengine wote wa Mikoa na Wilaya, kwani mfumo huu utakuwa na manufaa makubwa sana katika kuhifadhi na kuongeza ufanisi wa kazi za kiofisi, kwani wengi walikuwa wakipata changamoto nyingi katika uandaaji wa taarifa.

"Mnaporudi katika Mikoa yenu mkawe waalimu na mkawafundishe watumishi wengine yale yote mtakayofundishwa. Na ninaamini kwamba mtatoka hapa mkiwa na uwezo na mtautumia mfumo huu kwa ueledi na nidhamu ya hali ya juu"

Aliyasema hayo Mkurugenzi Kadushi wakati akifungua Mafunzo ya Utumiaji wa Mfumo wa Kielekitroniki wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika masuala ya Kesi kwa Makatibu Sheria na baadhi ya Mawakili wa Serikali wanaoshughulika na Takwimu yaliyoanza leo tarehe 5 Januari 2022 na kumalizika tarehe 8 Januari, 2022 Jijini Dar es salaam katika ofisi za TAGLA zilizopo Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

Aidha Mkurugenzi Kadushi alieleza kuwa mfumo huu unajukumu kubwa la kukusanya, kuchakata na kutunza taarifa zote zinazohusiana na uendeshaji wa kesi za Jinai nchini ambapo sehemu kubwa ya majukumu haya yanafanyika kwa mfumo wa zamani.

Pia Mkurugenzi aliishukuru Mamlaka ya Mtandao Serikali (eGA) kwa ushirikiano wao waliouonyesha katika mchakato wa uandaaji wa mfumo huu, kwani kwa kupitia Taasisi hiyo Serikali imefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba Taasisi za Serikali zinaongeza kasi ya kuhamishia majukumu yake katika mtandao.