Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

MIRADI YA UJENZI KUIMARISHA UTOAJI HUDUMA ZA MASHTAKA
20 Nov, 2026
MIRADI YA UJENZI KUIMARISHA UTOAJI HUDUMA ZA MASHTAKA

Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester Mwakitalu, amefanya ziara ya kutembelea miradi ya ujenzi wa majengo ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) katika Mkoa wa Kimashtaka Temeke na Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kukagua hali ya majengo hayo, kubaini changamoto zilizopo na kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo ili kuimarisha utoaji wa huduma za mashtaka kwa wananchi.

Ziara hiyo ilifanyika tarehe 15 Oktoba, 2026, ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka alieleza kuwa kwa sasa NPS inatoa huduma za mashtaka katika wilaya 93 nchini. Aidha, ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuiwezesha Ofisi hiyo kwa kujenga miundombinu ya ofisi, ambapo hadi sasa jumla ya majengo saba (7) ya ofisi za wilaya yamekamilika, hatua inayolenga kusogeza huduma za mashtaka karibu zaidi na wananchi.

Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Mashtaka aliambatana na timu ya Menejimenti ya NPS, ambapo alieleza kuwa miradi hiyo itasaidia kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao katika mazingira bora, hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuboresha huduma za mashtaka na haki jinai nchini.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Bw. Mwakitalu alisisitiza umuhimu wa kutunza majengo hayo, kudumisha usafi na kuzingatia utunzaji wa mazingira, ikiwemo upandaji wa miti, ili kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa safi na rafiki kwa watumiaji wa sasa na vizazi vijavyo.

Aidha, ameeleza kuwa ujenzi wa majengo hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha utendaji wa taasisi za haki jinai kwa kuboresha miundombinu ya utoaji huduma.