Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

“MIONGOZO YA MAAMUZI YA KUSHTAKI NA UTAIFISHAJI MALI ILETE TIJA KATIKA UTOAJI HAKI”– NAIBU DPP
01 Jul, 2026
“MIONGOZO YA MAAMUZI YA KUSHTAKI NA UTAIFISHAJI MALI ILETE TIJA KATIKA UTOAJI HAKI”– NAIBU DPP

Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Bibiana Kileo, amesema miongozo iliyohuishwa ya Maamuzi ya Kushtaki, Utaifishaji na Urejeshaji Mali pamoja na Mpango wa Kurejesha, Kutaifisha na Kusimamia Mali inapaswa kuleta tija, kuongeza ufanisi na kuboresha ubora wa utekelezaji wa majukumu katika taasisi za haki jinai.

Bi. Kileo ameyasema hayo tarehe 23 Juni, 2026 jijini Arusha wakati wa hafla ya uzinduzi wa miongozo hiyo, ambapo aliwashukuru wadau mbalimbali walioshiriki kikamilifu katika mchakato wa kuiboresha na kuihuisha. Alieleza kuwa maboresho yaliyofanyika yametokana na uzoefu wa utekelezaji wa miongozo ya awali na hitaji la kuimarisha usimamizi wa masuala ya utaifishaji, urejeshaji na usimamizi wa mali zinazotokana na uhalifu.

Amesema miongozo hiyo itasaidia kutatua changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika utekelezaji wa majukumu hayo na kuleta mfanano wa utendaji kazi miongoni mwa watendaji. Aidha, amewataka viongozi na watendaji wote kuhakikisha miongozo hiyo inatekelezwa kikamilifu na haitabaki kuwa nyaraka za kuwekwa kabatini bila kutumika.

Akizungumzia dhamira ya Serikali, Bi. Kileo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza katika kuboresha mfumo wa haki jinai kupitia maboresho ya sera, miundombinu na mazingira ya kazi ili kuwezesha utoaji wa huduma bora na haki kwa wananchi.

Amesisitiza umuhimu wa kufanya tathmini ya utekelezaji wa miongozo hiyo baada ya muda maalum ili kupima mchango wake katika kuimarisha utendaji kazi na kufikia matokeo yaliyokusudiwa. 

“Miongozo hii itakuwa na maana zaidi ikiwa italeta mabadiliko chanya katika usimamizi wa mali zinazotokana na uhalifu, kuongeza kasi ya utendaji na kuhakikisha haki inaonekana kutendeka kwa manufaa ya taifa letu.” Amesema Bi. Kileo. 

Sambamba na hayo Bi. Kileo ameeleza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu sheria zinazohusu utaifishaji wa mali ili kuongeza uelewa wa jamii na kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya uhalifu.