Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

MFUMO UTASAIDIA KUTATUA CHANGAMOTO MBALIMBALI ZA KIUTENDAJI - DPP
03 Mar, 2022
MFUMO UTASAIDIA KUTATUA CHANGAMOTO MBALIMBALI ZA KIUTENDAJI - DPP

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amesema kuwepo kwa mfumo wa kielekitroniki wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutasaidia kutatua changamoto nyingi za kiutendaji na hii ni kulingana na kuwepo kwa idadi kubwa ya mrundikano wa kesi katika Mahakama tangu mwaka 2000 kesi nyingi zinakuwa upelelezi wake bado haujakamilika.

"Tumekuwa na changamoto ya kupata taarifa za takwimu sahihi ya shughuli tunazozifanya hususani katika kujua idadi sahihi ya kesi zilizoendeshwa na kuisha mahakamani"

Amezungumza hayo Mkurugenzi wa Mashtaka wakati akifungua Mafunzo ya Utumiaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika masuala ya kesi kwa Waendesha Mashtaka wa Polisi, Mawakili wa Serikali, Makatibu Sheria pamoja na Watumishi wengine wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yaliyoanza tarehe 28 Februari, 2022 na kumalizika tarehe 29 Machi, 2022 Jijini Dar es Salaam katika ofisi za TAGLA zilizopo Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM)

Aidha, Mkurugenzi Mwakitalu alieleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yatasaidia katika ukusanyaji, uchakataji na utoaji wa taarifa mbalimbali za majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Mkurugenzi Mwakitalu alitoa shukrani zake kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa ufadhili wa kuwezesha mafunzo hayo. Na pia aliwashukuru wataalamu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Kitengo cha TEHAMA pamoja na wataalamu kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kutengeneza mfumo huu mzuri na kueleza kuwa mfumo huu ungeweza kununuliwa kwa gharama kubwa sana lakini wataalamu kutoka ndani wameweza kufanikisha hili.

Pia Mkurugenzi alitoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kuweka nguvu zaidi kujifunza kwa bidii ili wanaporejea katika vituo vyao vya kazi wakaanze kuutumia mfumo huo vizuri kwani utawasaidia katika utatuaji wa changamoto nyingi za kiutendaji. Na pia endapo kutakuwa na changamoto nyingine zitatokea wakati wakitumia mfumo huo basi wasisite kutoa taarifa kwa wakati.