Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

MENEJIMENTI ZA UTATU ZAFANYA TATHMINI YA UTENDAJI KAZI
20 Aug, 2025
MENEJIMENTI ZA UTATU ZAFANYA TATHMINI YA UTENDAJI KAZI

Menejimenti zinazounda Utatu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ( OTM), Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini(DCI),Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) zimekutana leo tarehe 18 Agosti, 2025 Jijini Dodoma kwa lengo la kufanya tathmini ya utendaji kazi baada ya kufanya ukaguzi katika mikoa yote nchini, kujadili changamoto zilizobainika ili kupata ufumbuzi wa changamoto zinazokwamisha utendaji kazi pamoja na kupanga mikakati ya kipindi kingine cha mwaka mmoja unaokuja.

Kikao kazi hicho ni mwendelezo wa vikao vya tathmini vinavyofanyika kila mwaka ambapo Menejimenti ya taasisi hizo hukutana na kujadiliana juu ya utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita pamoja na kupanga mikakati mipya.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao kazi hicho, Mkurugenzi wa Mashtaka ambaye ni Mwenyekiti wa Utatu huo Bw. Sylvester Mwakitalu amesema tangu kuanzishwa kwa umoja huo ufanisi wa utendaji  kazi  kwa kila taasisi kwa ngazi zote umeimarika, hususani malalamiko magerezani yanayohusu taasisi hizo yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Amesema,Umoja huu umewasaidia kupunguza muda wa kushughulikia majalada, upelelezi na uchunguzi unafanyika kwa muda mfupi, kesi zinafika mwisho na watu wanajua  hatma yao mapema hali inayopelekea uwepo wa wafungwa wengi kuliko mahabusu gerezani kwa sasa.

“Tunalo jukumu la kuimarisha ufanisi wa kazi zetu kwa kuweka imani ya kwamba hatumuonei mtu yoyote yule.” Amesema Mwenyekiti Mwakitalu

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI) Ramadhani Kingai amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuziwezesha taasisi za Haki Jinai ili ziweze kuwa na uwezo wa kukabiliana na uhalifu nchini.

Pia amesema kikao hicho kimekuja katika wakati muafaka ambapo nchi  inaelekea katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha kwamba maandalizi na mchakato mzima wa Uchaguzi yanafanyika katika mazingira yaliyo salama, amani na utulivu na hii inawapa wajibu kuimarisha ushirikiano wao, kuongeza kasi ya kudhibiti uhalifu wote na kuhakikisha kwamba wananchi wanatekeleza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi bila kuwa na hofu ama bugudha yoyote.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Bw. Crispin Chalamila amesema kupitia utatu huo amepata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wenzake na kupelekea kumrahisishia uongozi katika taasisi  yake kuwa rahisi na wenye tija. 

Pia Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Aretas Lyimo  amesema taasisi zao zimeungana ili kuhakikisha kwamba wanapambana na uhalifu ili kuleta amani na maendeleo ya kiuchumi nchini.

Aidha, kupitia mashirikiano yaliyopo katika umoja huo wa utatu ushindi wa kesi mahakamani umefikia zaidi ya asilimia 80 ikiwa ni matokeo ya kuungana na kufanya kazi kwa pamoja.

Akizungumza wakati akitoa salamu fupi Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Mhe. Mgeni Jecha ametoa shukrani zake kwa mwaliko walioupata wa kushiriki kikao hicho kwani imekuwa ni chachu ya maendeleo na ukuaji wa sekta ya Haki Jinai Tanzania na kupitia hilo wanapata uzoefu ambao wataenda kuutumia watakaporejea Zanzibar.