Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

MAWAKILI NA WACHUNGUZI WANOLEWA USHAHIDI WA KISAYANSI
20 Nov, 2026
MAWAKILI NA WACHUNGUZI WANOLEWA USHAHIDI WA KISAYANSI

Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Mkoa wa Tabora, kwa kushirikiana na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, imetoa mafunzo kwa wadau wa haki jinai kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa kisayansi katika maeneo ya vinasaba na baiolojia jinai, toksikolojia jinai na kemia jinai, kwa lengo la kuboresha uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka.

Mafunzo hayo yaliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Uhazili, Mkoa wa Tabora na kuwashirikisha wachunguzi na wapelelezi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Idara ya Uhamiaji pamoja na Mawakili wa Serikali kutoka NPS, Mkoa wa Tabora.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Tabora, Bi. Chema Maswi, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya ushahidi wa kisayansi katika uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka mahakamani, hususan katika kesi za mauaji na ukatili wa kijinsia.

“Matumizi ya ushahidi wa kisayansi yana nafasi kubwa katika kuthibitisha makosa mahakamani. Hata hivyo, ni muhimu kuhakikisha sampuli zinachukuliwa na kutunzwa kwa usahihi ili kuepuka changamoto zinazoweza kuathiri matokeo ya uchunguzi na uwasilishaji wa ushahidi mahakamani,” amesema Bi. Maswi.

Mafunzo hayo yalitolewa na Dkt. Fidelis Bugoye, Meneja wa Maabara ya Uchunguzi wa Vinasaba na Baiolojia; Dkt. Kagera Ng’weshemi, Meneja wa Maabara ya Toksikolojia; pamoja na Bi. Joyce Njisya, Meneja wa Maabara ya Kemia. Wataalamu hao waliwawezesha washiriki kuelewa kwa kina taratibu za uchunguzi wa kisayansi, hususan uchukuaji na utunzaji sahihi wa sampuli za vinasaba, kemia na toksikolojia.

Aidha, washiriki walipata fursa ya kufanya mazoezi kwa vitendo kuhusu namna sahihi ya kuchukua na kuhifadhi sampuli mbalimbali ili kulinda ubora na uaminifu wa ushahidi na kupunguza makosa yanayoweza kuathiri matokeo ya uchunguzi.

Akifunga mafunzo hayo, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Tabora, SP Mbaruk Msonga, amewahimiza washiriki kutumia na kusambaza elimu waliyoipata kwa wadau wengine, huku akitoa wito wa kuendelezwa kwa mafunzo hayo ili kuboresha utendaji kazi wa wadau wa haki jinai.