MAHABUSU WAMPONGEZA DPP KWA KUPUNGUZA MSONGAMANO SEGEREA
Mahabusu na wafungwa kutoka Gereza la Mahabusu Segerea wamempongeza Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu kwa kupunguza msongamano wa Mahabusu na wafungwa waliopo katika gereza hilo tofauti na hali ilivyokuwa awali.
“Mwaka 2021 ulipotutembelea katika gereza hili tulikuwa mahabusu na wafungwa zaidi ya elfu mbili lakini leo mahabusu na wafungwa idadi yetu ni mia tisa na kidogo, kwa kweli tunakushukuru sana kwa kushughulikia kesi zetu na kufanya mrundikano kupungua humu gerezani”.
Mahabusu na Wafungwa wamebainisha hayo wakati Mkurugenzi wa Mashtaka alipofanya ziara ya kutembelea gereza hilo kwa lengo la kuongea na kusikiliza kero za mahabusu na wafungwa hao.
Kwa upande wake Bw. Mwakitalu ameeleza kuwa licha ya kazi nzuri inayofanywa katika mkoa wa Dar es saalam, bado inatakiwa kuongeza kasi ya ukamilishaji wa upelelezi na uendeshaji wa mashtaka na kuhakikisha kesi zinazopelekwa mahakamani zinakuwa zenye ushahidi utakaoleta ushindi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Crispin Chalamila alisisitiza juu ya kuongeza kasi katika kushughulikia kesi kwa wakati ili kuepusha malalamiko huku akihimiza kuwa haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa.
Aidha, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Aretas Lyimo alisema kuwa kesi zinazohusiana na madawa ya kulevya ambazo upelelezi haujakamilika aliahidi kuzishughulikia na kukamilisha upelelezi wake kwa wakati.