KIFO CHA MTUMISHI RHOIDA CHAACHA PENGO

Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imepata pengo kubwa kutokana na kifo kilichotokea kwa aliyekuwa Mtumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka marehemu Rhoida Augustine Kisinda kilichotokea mnamo tarehe 4 Mei, 2025 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara alipokuwa akipatiwa matibabu.
Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi ya kumuaga Marehemu huyo yaliyofanyika tarehe 7 Mei, 2025 Mkoani Manyara, Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema marehemu alikuwa ni mtumishi Hodari, mwaminifu, muadilifu na mchapakazi hivyo kama ofisi imepata pengo kubwa sana kwao ambalo sio rahisi kuliziba.
"Tunaweza kupata kibali cha kuajiri mtu mwingine lakini anaweza asizibe pengo la Rhoida." Amefafanua Mkurugenzi Mwakitalu.
Aidha, Mkurugenzi Mwakitalu kwa niaba ya Watumishi wote wa Ofisi ya Taifa ya ametoa pole kwa familia yote ya marehemu Rhoida kwa msiba huo mkubwa na kuahidi kuungana pamoja nao, kuwaombea na kuwapa faraja ya kweli katika kipindi chote cha majonzi.
Pia amewashukuru wadau mbalimbali wakiwemo Mahakama, TAKUKURU, Jeshi la Polisi, Chama cha Mawakili Tanganyika, Uhamiaji, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na waombelezaji wengine walioungana pamoja nao kushiriki kwenye ibada ya mazishi ya kumuaga Marehemu Rhoida.
Kwa upande wake Mkuu wa Jimbo la KKKT Babati Mchungaji Robert Mallya amewaasa waombelezaji hao kutenda haki na kuzingatia maadili katika maeneo yao ya kazi.