KAIMU MKURUGENZI MSIGWA ASISITIZA JUU YA UMUHIMU WA UTOAJI WA TAARIFA SAHIHI.

Kaimu Mkurugenzi Divisheni ya Makosa ya Udanganyifu na Utakasishaji Fedha Bw. Christopher Msigwa amesisitiza juu ya umuhimu wa utoaji wa taarifa zilizo sahihi ambazo zitasaidia katika suala zima la takwimu.
Kaimu Mkurugenzi Msigwa ameyasema hayo wakati akifungua Kikao Kazi cha Maafisa Viunganishi (focal persons) wa Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili kinachofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Novemba, 2024 mkoani Morogoro.
Kikao Kazi hicho kinajumusha Maafisa Viunganishi kutoka Mikoa 30 ya Kimashtaka pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Kikosi Kazi cha Taifa cha Kupambana na Ujangili (NTAP), Kikosi Kazi cha Taifa cha Kupambana na Makosa ya Madini na Kituo cha Kupambana na Uhalifu wa Kifedha na Uhujumu Uchumi (ECC).
Aidha Kaimu Mkurugenzi Msigwa amesema taarifa wanazozihitaji katika Kikao Kazi hicho kutoka kwa Maafisa Viunganishi hao ni muhimu sana kwao kama Idara na kwa ajili ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ujumla.
Pia amebainisha kuwa lengo la taarifa hizo ni pamoja na kuwasaidia katika masuala mbalimbali ikiwemo kujua aina ya mafunzo wanayopaswa kuyatoa kama yale yanayohusu uratibu wa upelelezi na uendeshaji wa mashtaka yenye viashiria vya mazalia ya uhalifu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili Bw. Salimu Msemo ameeleza Kikao Kazi hicho kinalenga kuwakutanisha Maafisa Viungo wa Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili ili kuwajengea uelewa wa pamoja kwa mujibu wa sheria na miongozo.
Aidha, aliongeza kuwa, lengo jingine ni kuandaa Taarifa ya Taifa ya Takwimu zinazohusiana na Makosa ya Mazingira na Maliasili,
"Jambo lolote la msingi haliwezi kufanyika bila kuwa na takwimu sahihi, ambapo washiriki hawa walianza kulifanyia kazi eneo hili la ukusanyaji wa taarifa kabla ya kuja kushiriki kwenye Kikao Kazi hiki." Amesema Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Msemo.
Alieleza zaidi kuwa, lengo jingine ni kupata maoni kuhusiana na Mpango Mkakati wa Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili ambao upo katika hatua za awali.
Aidha, Kikao Kazi hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Divisheni ya Utaifishaji Mali, Makosa yanayovuka Mipaka na Uhalifu Mahsusi Bw. Faraja Nchimbi, Mkurugenzi Divisheni ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi Bi. Javelin Rugaihuruza, Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Usimamizi wa Kesi na Uratibu wa Upelelezi Bw. Saraji Iboru, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Rushwa Bw. Zakaria Ndaskoi na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Udanganyifu na Utakasishaji Fedha Bw. Seth Mkemwa ambao kwa pamoja walisisitiza masuala mbalimbali yakiwemo;
1. Maafisa Viunganishi kutimiza wajibu wao na kutekeleza majukumu yao kama walivyoelekezwa ili kuleta tija katika utendaji wa Idara na Taasisi kwa ujumla;
2. Kuhakikisha wanazingatia matumizi ya mfumo wa sasa na baadaye mfumo ulioboreshwa ili kuboresha upatikanaji wa taarifa na kuimarisha upatikanaji wa matokeo chanya katika uendeshaji wa mashauri mahakamani; na
3. Kuwashirikisha Maafisa Viunganishi wa Idara nyingine na watumishi wengine kwa ujumla katika Mikoa yao masuala muhimu watakayojifunza kutoka kwenye Kikao Kazi hiki.