Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

JELA MIAKA 30 KWA KOSA LA KUKUTWA NA DAWA ZA KULEVYA
03 Jul, 2025
JELA MIAKA 30 KWA KOSA LA KUKUTWA NA DAWA ZA KULEVYA

Mahakama ya Wilaya Mkoa wa Mbeya imemuhukumu Kessy Mwalingo kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Hukumu hiyo imesomwa tarehe 30 June, 2025 na Hakimu Paul Rupia baada ya kuridhika na Ushahidi uliowasilishwa na upande wa Mashtaka.

Katika kesi hiyo Na. 10190 ya Mwaka 2025, Bw. Kessy Mwalingo ambaye ni mkazi wa Iziwa iliyopo ndani ya Wilaya na Mkoa wa Mbeya alikuwa anakabiliwa na shtaka moja la kukutwa na Dawa za Kulevya Kinyume na Kifungu cha 15A (1)(2)(c) ya Sheria ya Kuzuia na Kudhibiti Madawa ya Kulevya (Sura ya 95 Marejeo ya Mwaka 2019).

Mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo tarehe 6 Machi, 2025 katika maeneo ya Iziwa iliyopo ndani ya Wilaya na Mkoa wa Mbeya ambapo imethibitika kuwa mshtakiwa alikutwa na mfuko wa Sandalaus mweupe wenye majani makavu na mbegu yaliyo thibitishwa kuwa ni Cannabis Sativa "Bhangi" 

Siku ya tukio majira ya Saa 9 Alasiri upekuzi ulifanyika nyumbani kwa mshtakiwa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mwananchi mmoja kuwa ameibiwa maharage na mshtakiwa. Walipofika nyumbani kwa mshtakiwa walimuuliza kuhusiana na tuhuma za kuiba maharage na alikana kutenda kosa hilo kisha Mwenyekiti na Mgambo walimuomba mshtakiwa wafanye upekuzi nyumbani kwake ambapo aliwakubalia na ndipo katika upekuzi huo walikuta mfuko wa Sandalaus mweupe. Mshtakiwa alipoulizwa kuhusu mfuko huo alidai kuwa ni majani ya kuwashia moto na walipofungua mfuko huo walikuta majani makavu na mbegu zidhaniwazo kuwa ni bhangi. 

Mwenyekiti wa Mtaa wa Iziwa na Mgambo wa Mtaa walimkamata mshtakiwa pamoja na kielelezo alichokutwa nacho na kumfikisha Kituo cha Polisi cha Kati Mbeya kwa hatua zaidi za Kisheria.

Jumla ya mashahidi saba (7) wa upande wa mashtaka walitoa ushahidi na mtuhumiwa alijitetea mwenyewe.

Kesi hii imeendeshwa na mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Mbeya.