Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

DPP Azindua Tovuti ya Chama cha Waendesha Mashtaka wa Afrika Mashariki
16 Nov, 2020
DPP Azindua Tovuti ya Chama cha Waendesha Mashtaka wa Afrika Mashariki

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga leo tarehe 16 Novemba, 2020 amefanya uzinduzi wa Tovuti ya Chama cha Waendesha Mashtaka wa Afrika Mashariki akishirikiana na viongozi wengine kutoka katika chama hicho.

Mkurugenzi wa Mashtaka amefanya uzinduzi huo kwa njia ya mtandao akiwa Jijini Dodoma akiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Kenya ambaye pia ni Katibu wa chama hicho Bw. Noordin Mohamed Haji pamoja na Bi. Heather Schildge ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa Misheni kutoka Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani - USAID, Bi. Julie Thomson, Mkurugenzi wa Trafiki Programu ya Afrika, Wawakilishi kutoka katika Mashirika ya Kimataifa na Kikanda pamoja na Waendesha Mashtaka kutoka katika baadhi ya nchi wanachama wa umoja huo.

Akizindua tovuti hiyo Bw. Biswalo Mganga alisema uzinduzi wa tovuti ni miongoni mwa hatua muhimu iliyofikiwa katika kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa wanyamapori katika nchi za Afrika Mashariki.

Chama cha Waendesha Mashtaka wa Afrika Mashariki kilianzishwa mwaka 2010 kikiwa na jumla ya wanachama wa nchi tano zikiwapo Tanzania, Rwanda, Burundi, Sudani ya Kusini na Kenya. Hadi kufikia hivi sasa chama hicho kimefanikiwa kuongeza wanachama kutoka nchi nyingine jirani zikiwemo Somalia, Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Sudan, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi na Msumbiji.

Wakati wa Uzinduzi huo Mkurugenzi wa Mashtaka aliendelea kueleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2009 hadi 2014 katika nchi ya Tanzania idadi nyingi ya Tembo ilishuka hadi kufikia asilimia 60 kutokana na ujangili pamoja na biashara haramu ya wanyamapori ukilinganisha na matukio ya nchi nyingine za jirani.

Tovuti hii ni chombo muhimu kwa ajili ya kuhakikisha masuala yote ya taarifa dhidi ya uhalifu wa Wanyama katika ngazi za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa yanarahisishwa ili kupambana na wale wote wanaojihusisha na biashara haramu za wanyamapori pamoja na kuimarisha mfumo wa mawasiliano katika nchi wanachama.

"Ni matumaini yangu kuwa tovuti hii kupitia umoja wa Waendesha Mashtaka wa masuala ya wanyama na mazingira utaamsha katika matumizi ya sheria mbalimbali za Kikanda za wanyama kupelekea kukua kwa uhifadhi wa wanyama na kuwa na kituo cha kutolea taarifa kuhusu makosa hayo.

" Napenda kuwashukuru Waendesha Mashtaka wote kwa ushirikiano waliotoa katika kutengeneza na kuanzisha tovuti na juhudi za makusudi za kujenga umoja huu".

Mwisho Mkurugenzi wa Mashtaka aliwashukuru wajumbe wote waliohudhuria katika kikao hicho wakiwemo Bw. Noordin Mohamed Haji, Bi. Heather Schildge, Bi. Julie Thomson, na wawakilishi kutoka Mataifa mbalimbali ya kiserikali.