Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

DPP AWATAKA WATUMISHI WA OTM KUFANYA KAZI KWA BIDII NA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA.
25 Jan, 2024
DPP AWATAKA WATUMISHI WA OTM KUFANYA KAZI KWA BIDII NA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA.

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (OTM) kufanya kazi zao kwa bidii na kuzingatia weledi wa taaluma yao ikiwemo kufanya kazi kwa uaminifu ili kutenda haki kwa umma.

Mwakitalu ametoa rai hiyo mapema leo Januari 25, 2024 katika ukumbi wa hoteli ya Lenana ya Jijini Mwanza wakati akifungua mkutano wa baraza la kwanza la mwaka la wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka lililojumuisha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi.

Bw. Mwakitalu amesema katika kipindi cha mwaka mmoja,Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeweza kufikia sehemu kubwa ya utekelezaji wa malengo iliyokuwa imejiwekea  yakiwepo masuala ya mashauri ya jinai kuendeshwa na kutolewa maamuzi kwa haraka na kupelekea kupungua kwa mrundikano wa kesi za muda mrefu katika mahakama nyingi nchini.

Katika hatua nyingine Mwakitalu ameeleza kuwa kutokana na kuimarika kwa utendaji wa watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kumesaidia kupunguza mrundikano wa mahabusu  katika magereza mbalimbali nchini pamoja na kupungua kwa malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na wananchi kwa njia mbalimbali ikiwemo barua pepe, simu na wengine kufika ofisini.

Amesema, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeundwa ili kurahisisha utoaji wa huduma za mashtaka kwa wananchi kwa kuwezesha kesi nyingi kuendeshwa kwa wakati  na kuhakikisha haki inatendeka kwa lengo la kuwepo kwa haki, amani na usalama katika nchi yetu.

Aidha, Mwakitalu amesema katika kuhakikisha watumishi wote wanafanya kazi zao kwenye mazingira salama, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeendelea kutekeleza   miradi mbalimbali ya majengo ya ofisi za mikoa 10 ambapo mikoa miwili kati yake imekamilika ikiwemo mkoa wa Pwani na Ilala eneo la Kinyerezi ambapo mwishoni mwa mwezi Januari, 2024, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inatarajiwa  kupokea majengo ya Ofisi kutoka mikoa ya Shinyanga na Manyara.

Bw. Mwakitalu amesema kuwa mpaka sasa jumla ya ofisi 92 za mashtaka zimefunguliwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mikoa 30 ya kimashtaka na wilaya 62 za Tanzania Bara ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya ofisi katika kusogeza huduma za kimashtaka karibu na wananchi.Vile vile Mwakitalu amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka itaendelea kufungua ofisi katika wilaya 47 zilizobaki ili kuendelea kutoa huduma bora kwa watanzania wenye kesi mbalimbali.

Naye Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambaye ni Afisa Tawala Mkuu Bw.Juma Katanga amesema kikao cha Baraza la Wafanyakazi cha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kinalenga katika kujadili na kupitia Mipango na Makisio ya Mapitio ya bajeti katika kipindi cha nusu mwaka kuanzia Julai 2023 hadi Januari, 2024.

Katanga amesema wafanyakazi wa OTM bado wanakabiliwa na baadhi ya changamoto zikiwepo uhaba wa wafanyakazi katika maeneo mbalimbali, upungufu wa vitendea kazi katika ofisi nyingi za wilaya zilizofunguliwa hivi karibuni huku akisema kuwa Baraza la Wafanyakazi limekuwa sehemu ya msukumo kwa menejimenti kupunguza baadhi ya changamoto ikiwemo kununua magari mapya, kuajiri  watumishi pamoja na kununua samani za ofisi katika Wilaya na Mikoa.

Wakati huohuo,   Katanga ameiomba Serikali kuona namna ya kuongeza bajeti katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutokana na majukumu nyeti inayoyatekeleza kwa Maendeleo ya Taifa  ikiwemo kupatikana kwa nyumba za wafanyakazi zitakazosaidia kuishi katika mazingira salama.

“Mfano Wakili wa Serikali anaendesha kesi za Ugaidi,Ujambazi, Masuala ya pesa haramu alafu anaishi kwenye nyumba ya kupanga pengine ni ya jambazi  fikiria jinsi mazingira hayo yalivyo hatari, serikali inapaswa kuliona hili kwa jicho la zaidi” amesema Katanga

Awali akizungumza kabla ya ufunguzi wa mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi.Javelin Rugaihuruza amesema mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashataka ulikusudiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2023   lakini kutokana na sababu zilizojitokeza nje ya uwezo wa taasisi ulishindwa kufanyika na umefanyika leo tarehe 25 mwezi Januari 2024.