Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

DPP AWATAKA MAKATIBU SHERIA KUJIEPUSHA NA RUSHWA
08 Feb, 2021
DPP AWATAKA MAKATIBU SHERIA KUJIEPUSHA NA RUSHWA

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw.Biswalo Mganga amewataka Makatibu Sheria nchini kuhakikisha wanatumia vizuri mfumo mpya wa Ukusanyaji, Uchakataji, Utumaji na Utunzaji wa Takwimu za Kesi za Jinai, na Kumbukumbu za Makosa ya Rushwa kwa njia ya Kidijitali hali itakayowezesha utoaji wa Takwimu sahihi kwa maendeleo ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga wakati akifunga Mafunzo ya siku 6 ya Makatibu Sheria kutoka Mikoa yote ya Tanzania bara mafunzo yaliyofanyika Manispaa ya Singida yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo makatibu hao katika Ukusanyaji, Uchakataji, Utumaji na Utunzaji wa Takwimu za Kesi za Jinai, na Kumbukumbu za Makosa ya Rushwa kwa mfumo wa Kidijitali.

Ameeleza kuwa jukumu la watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni kuwajibika kwa umma na serikali hivyo Makatibu Sheria wanalo jukumu kubwa la kuhakakikisha huduma bora za mashtaka zinawafikia wananchi na kuiona ofisi kuwa yao.

“Naomba niseme jukumu kubwa tulilonalo ni kuwajibika kwa Umma, Taasisi na Serikali kwa kuhakikisha tunatoa huduma bora na za kuvutia kwa wananchi, nisingependa kusikia lugha mbaya toka kwenu zikiwahusu watu wanaokuja kwenu kutafuta msaada badala yake tumieni lugha nzuri kwani majalada yote yanapitia kwenu”

Biswalo amesema Makatibu Sheria ndiyo mlango wa Kupokea majalada hivyo wasiwe chanzo cha kujihusisha na vitendo vya rushwa kwani kufanya hivyo kunadhoofisha maendeleo ya Nchi na Taifa kwa ujuma

“Sitaki kusikia ninyi Makatibu Sheria mnakuwa vyanzo vya kujihusisha na vitendo vya Rushwa ndani ya taasisi kwa sababu tu watu wote wanaanzia kwenu na wala msidanganyike kwani mkifanya hivyo mtaishia pabaya, siko tayari kumvumilia mtu anayekula Rushwa”

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Biswalo amewaasa watumishi hao kutoharibu taaluma yao ya Ukatibu Sheria kwa kujihusisha na uvujishaji wa siri za Nyaraka za Ofisi kwani kufanya hivyo ni kinyume cha maadili pia hali ambayo inahatarisha usalama wa nchi.

“Niwaombe ninyi Makatibu Sheria mnayo nafasi kubwa ya kutupatia na kusaidia taarifa za siri juu ya watu wanaofutilia majalada yetu hususani makanjanja ili tumfahamu mtu anayefuatilia ana lengo gani na tujue tunaanzia wapi kumchukulia hatua”

Aidha, Biswalo akizugumzia suala la Mfumo mpya wa Ukusanyaji,Uchakataji, Utumaji na Utunzaji wa Takwimu za Kesi za Jinai, na Kumbukumbu za Makosa ya Rushwa kwa mfumo wa Kidijitali amewataka kuhakikisha taarifa zinaingizwa kwenye mfumo kwa uhakika na umakini huku akiwaonya Makatibu hao kwenda kufanya kazi zao kwenye internet Café ambako nyaraka za serikali husalia na kuhataraisha usalama wa ofisi na nchi kwani watu wabaya wanaweza kuzitumia kwa maslahai yao binafsi.

“Ni marufuku kutumia barua pepe za Ofisi kwenye Kompyuta za internet café utumike ndani ya ofisi na Kompyuta za ofisi tu kwani kutumia huko taarifa zinabaki na watu wanaanza kudukua hivyo kwa hili atakayebainika sitamwonea huruma lazima hatua kali zichukulie dhidi yake”

Biswalo ameongeza kuwa utumiaji wa mfumo huo mpya wa Uchakati na utumaji wa taarifa isiwe sababu ya kuachana na mfumo wa zamani wa regista ambapo amesisitiza mifumo yote kwenda samabmba hadi pale mfumo wa kidijitali utakapokuwa umeimarika na kusimama vizuri

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Kesi na Uratibu wa Upelelezi Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambaye anashughulikia Usimamizi wa Kesi Bw. Tumaini Kweka amesema kuwa Makatibu Sheria ni watu muhimu sana hivyo mafunzo hayo yamejikita kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa viwango vinavyotarajiwa pamoja na kuwawezesha kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo

“Naomba kukutaarifu kuwa mafunzo haya yameshirikisha washiriki 30 kutoka Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara hivyo tuna imani kuwa kile walichojifunza hapa kinaenda kuwa chachu kubwa kwa wengine waliosalia kwenye maeneo yao”

Kweka ameongeza kuwa katika mafunzo hayo jumla ya Mada nane zimewailishwa kutoka kwa watalaamu wa ndani na nje ya taasisi hiyo waliowasilisha mada kwa kina na washiriki kupata nafasi ya kuuliza maswali na kujibiwa”

Naye mwakilishi wa washiriki wa Mafunzo hayo ya Ukusanyaji,Uchakataji, Utumaji na Utunzaji wa Takwimu za Kesi za Jinai, na Kumbukumbu za Makosa ya Rushwa kwa njia ya Kidijitali Bi Faraja amesema kuwa mafunzo hayo kwao ni chachu kubwa ya kuboresha utendaji kazi wao hususani kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushirikiano wa Idara ya Usimamizi wa Kesi na uratibu wa upelelezi na Programu ya BSAAT kupitia Divisheni ya Makosa ya Udanganyifu, Utakatishaji fedha na Rushwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.