DPP AMEWATAKA MAWAKILI KUZINGATIA HAKI ZA WATOTO
Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu awataka Mawakili wa Serikali kufanya kazi zao kwa umakini, kupitia majalada yote kwa umakini ili kuweza kulinda haki za watoto.
Mkurugenzi wa Mashtaka akizungumza hayo wakati akifungua Mafunzo na maelekezo ya utekelezaji wa ukaguzi wa vizuizi vya watoto wanaokinzana na sheria ambayo yamedhaminiwa na Shirika la Kimataifa la Watoto (UNICEF) yanayofanyika leo tarehe 15 Novemba, 2021 katika Ukumbi wa Rafiki Hotel Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mwakitalu alieleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inayo jukumu la kusimamia haki jinai kwa maana ya kuendesha kesi za jinai, lakini katika Uendeshaji wa Mashtaka hayo, ofisi ina jukumu pia la kuratibu Upelelezi, na pia kufanya ukaguzi kwenye mahabusu, magereza na mahala pengine ambapo washtakiwa wa uhalifu wanatunzwa.
Mwakitalu aliendelea kueleza kuwa mafunzo hayo pia yataongeza tija kwenye utendaji wa kazi, na pia lile kundi la Watoto wanaokinzana na sheria au wale ambao ni waanga ni kundi muhimu sana katika utendaji wa kazi za ofisi hii.
Aidha alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwasababu yatasaidia kuhakikisha kuwa haki za watoto za zinalindwa, na pia kupata uelewa utakaowezesha kufanya maamuzi sahihi na kuchukua hatua stahiki katika haki za watoto.
Nae pia Kaimu Mkurugenzi Divisheni ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi Bw. Tumaini Kweka alieleza kuwa mafunzo hayo ni ya kwanza katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambayo yamewakutanisha kushughulikia mashauri katika ofisi za mikoa na wilaya. Na lengo la mafunzo hayo ni kuboresha na kuweka namna bora ya jinsi ya kuendesha mashauri hayo Mahakamani na vilevile kuona namna bora ya kushughulika na kesi zinazowahusu watoto ambao wamekinzana na sheria.
"Dhima au lengo kuu la mafunzo haya ni kuwajengea uelewa wa pamoja juu ya utaratibu mzuri wa kukagua magereza, kukagua mahabusu za polisi na mahabusu za watoto ambao wamekinzana na sheria wanakuwa wamehifadhiwa." Akizungumza hayo Mkurugenzi Kweka.