DPP AIPONGEZA MENEJIMENTI YA NPS KWA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu ameipongeza Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa utekelezaji mzuri wa majukumu ya Divisheni na Vitengo katika mwaka wa fedha 2025/2026, hatua inayowezesha Taasisi kufikia shabaha na malengo yaliyoainishwa katika Mpango Mkakati na kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za mashtaka kwa wananchi. Aidha, amepongeza watumishi wa NPS kwa uwajibikaji wao katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
Akizungumza wakati wa kikao cha Menejimenti kilichofanyika tarehe 25 Juni, 2026, jijini Arusha, Bw. Mwakitalu alipokea na kujadili taarifa za utekelezaji zilizowasilishwa na Divisheni na Vitengo mbalimbali, ambazo zilionesha shughuli zilizotekelezwa pamoja na matumizi ya fedha kwa mujibu wa Mpango Mkakati (SP) katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2026.
Katika kikao hicho, Menejimenti ilijadili mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na mikakati ya kuendelea kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Taasisi kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa katika Mpango Mkakati wa NPS. Pia Wakuu wa Divisheni na Vitengo walihimizwa kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za mashtaka kwa wananchi.
" Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya. Mafanikio haya yanatokana na ushirikiano, uwajibikaji na kujituma kwa kila mmoja wenu. Ni muhimu watumishi kutumia kwa ufanisi mifumo mbalimbali ya kidijitali, hususan Mfumo wa Usimamizi wa Kesi (CMIS), katika utekelezaji wa majukumu yetu ili kuwa na kumbukumbu sahihi, kuongeza uwajibikaji na kuboresha ufanisi wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati," alisema Bw. Mwakitalu.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa Menejimenti kuazimia kuendelea kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya Divisheni na Vitengo, kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za Taasisi na kuendeleza matumizi ya teknolojia ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
