WAZIRI HOMERA AIPONGEZA NPS KWA KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MAHABUSU MAGEREZANI
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera, ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na ufanisi, hali iliyochangia kupungua kwa msongamano wa mahabusu katika magereza mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yaliyopo Njedengwa, Jijini Dodoma, tarehe 26 Novemba 2025, Dkt. Homera alisema hatua ya NPS kusimamia mashauri ya jinai kwa haraka na umakini imeleta maboresho makubwa katika mfumo wa utoaji haki.
“Hali imebadilika chini ya Serikali ya Awamu ya Sita na chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka Bw.Sylvester Mwakitalu, kwa sasa msongamano wa mahabusu magerezani umepungua kwa kiasi kikubwa, nilipotembelea gereza la Mbeya niliweza kujionea hali ilivyobadilika,” alisema Waziri Homera.
Pia aliipongeza NPS kwa kuendeleza ushirikiano mzuri na vyombo vya upelelezi na uchunguzi nchini, hali inayochangia kuharakisha upelelezi wa kesi za jinai.
“Nimeona mkishirikiana vizuri na Jeshi la Polisi, TAKUKURU, DCEA, lakini pia TRA katika kushughulikia kesi mbalimbali za kiuchumi,” aliongeza Dkt. Homera
Waziri Homera aliitaka NPS kuendeleza weledi na uadilifu katika kusimamia mashauri ya jinai ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati, akibainisha kuwa mashauri mengi yana maslahi mapana kwa taifa.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuyapa kipaumbele matumizi ya teknolojia katika utendaji wa taasisi, akieleza kuwa mifumo ya TEHAMA ni nyenzo muhimu katika kuharakisha utoaji wa haki.
“Mifumo ya TEHAMA iwe kipaumbele chenu ili mifumo yenu na ile ya Mahakama iweze kusomana, na hivyo kuwasaidia wananchi kupata haki kwa wakati,” alisisitiza Waziri Homera.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu, alimshukuru Waziri na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria kwa kufanya ziara yao ya kwanza katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka tangu walipoteuliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
DPP, Mwakitalu alieleza kuwa Serikali imetoa mchango mkubwa katika kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo. Huku akibainisha kuwa NPS imepiga hatua kubwa katika kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia upanuzi wa ofisi zake nchini.
“Kwa sasa NPS ina ofisi za mikoa kote nchini, na kwa ngazi ya Wilaya zimebaki wilaya 21 ambazo maandalizi ya kuanzisha ofisi katika maeneo hayo tayari yameanza,” alisema DPP Mwakitalu.
Sambamba na hayo Bw. Mwakitalu alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imewezesha ongezeko la watumishi kwa kutoa kibali cha kuajiri, ambapo idadi ya watumishi imeongezeka kwa kiwango kikubwa sana ikilinganishwa na mwaka 2021, hatua iliyowezesha kuimarika kwa utoaji wa huduma.
Katika Ziara hiyo Waziri Homera aliambatana pia na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Zainabu Katimba na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Franklin Rwezimula.