DKT. HOMERA APONGEZA USIMAMIZI MZURI WA UJENZI WA JENGO LA NPS MKOA WA SINGIDA
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, amefanya ziara ya kikazi katika mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Mkoa wa Singida, kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo muhimu unaotekelezwa na Serikali.
Ziara hiyo imefanyika tarehe 9 Januari 2026, ambapo Waziri Dkt. Homera amepata fursa ya kukagua hatua mbalimbali za ujenzi wa jengo hilo na kujionea maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa.
Akizungumza mara baada ya kufanya ukaguzi huo, Dkt. Homera amempongeza Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu, pamoja na uongozi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa usimamizi mzuri wa mradi huo unaolenga kuboresha utoaji wa haki kwa wakati.
Dkt. Homera amesema kukamilika kwa jengo hilo kutaboresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya kazi kwa Waendesha Mashtaka mkoani Singida, hatua itakayoongeza ufanisi, uwajibikaji na kasi ya utoaji wa huduma za mashtaka kwa wananchi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili, kwa kuzingatia thamani ya fedha za umma zilizotolewa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu, amemshukuru Dkt. Juma Homera kwa ushirikiano unaotolewa na Wizara ya Katiba na Sheria katika kuboresha miundombinu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Mwakitalu ameeleza kuwa ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha utendaji wa taasisi za haki jinai na kuhakikisha huduma za mashtaka zinawafikia wananchi kwa karibu zaidi.
Bw. Mwakitalu ameongeza kuwa mara baada ya kukamilika, jengo hilo litasaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa ofisi, kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za mashtaka kwa wananchi mkoani Singida.
