Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

WAZIRI AMEITAKA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA KUFANYA KAZI KWA UFANISI MKUBWA ZAIDI.
18 Oct, 2021
WAZIRI AMEITAKA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA KUFANYA KAZI KWA UFANISI MKUBWA ZAIDI.

Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi ameitaka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuhakikisha upelelezi wa makosa ya Jinai kuhusiana na misitu na wanyamapori unaratibiwa vizuri, watuhumiwa wanafikishwa mahakamani na Mashtaka yanaendeshwa kwa ufanisi mkubwa kwa lengo la kutokomeza ujangiri, kulinda rasilimali zetu na kuikuza sekta ya utalii na uhifadhi nchini.

"Ninafurahi kuona mafunzo haya ninayofungua leo yamejumuisha wadau wote muhimu katika mfumo wa upelelezi na Uendeshaji wa makosa ya Jinai yahusuyo misitu na wanyamapori. Hivyo, sina shaka kwamba, mafunzo haya yatakuwa chachu ya mabadiliko na mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya ujangiri na ulinzi wa maliasili zetu." Akizungumza hayo Profesa Kabudi wakati akifungua mafunzo ya upelelezi na Uendeshaji wa Kesi za wanyamapori na misitu yanayofanyika Mkoani Morogoro katika Ukumbi wa Nashera Hotel.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ameeleza kwamba kumekuwa na ongezeko la makosa ya wanyapori na mazao ya misitu nchini hivyo mafunzo haya kwao yana tija katika kulinda maslahi ya Taifa.

Akifafanua ukubwa wa tatizo hilo, Bw. Mwakitalu amesema kuwa katika kikao cha Mahakama ya Rufaa kilichoanza leo tarehe 18 Oktoba, 2021 Musoma mkoani Mara, imebainika kuwa kuna kesi 18, ambapo kesi 14 kati ya hizo ni za wanyamapori na misitu.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Rosemary Shio alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo na kuwapatia ujuzi utakao wawezesha kupeleleza na kuendesha kesi za wanyamapori na misitu kwa weledi na uadilifu.