WATUMISHI WA OTM WAJENGEWA UWEZO KATIKA MASUALA YA ITIFAKI NA USTAARABU

Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (OTM) wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu masuala ya Itifaki na Ustaarabu. Mafunzo hayo yalilenga kuwapatia washiriki uelewa mpana kuhusu taratibu za kiitifaki, mawasiliano ya kitaaluma, pamoja na namna ya kudumisha ustaarabu katika utekelezaji wa majukumu ya kikazi, ndani na nje ya taasisi.
Mafunzo hayo yalifanyika kuanzia tarehe 13 hadi 17 Oktoba 2025, na kuendeshwa na Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (zamani Chuo cha Diplomasia), Jijini Dar es salaam.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Dkt. Antonio Kimambo, Mkuu wa Idara ya Utafiti, Kozi Fupi, Ushauri wa Kitaalamu na Programu Maalum katika kituo hicho, alisema kuwa uelewa wa masuala ya itifaki ni nguzo muhimu katika kujenga taswira chanya ya utumishi wa umma na taifa kwa ujumla.
“Utendaji wenye kuzingatia ustaarabu na itifaki sahihi ni ishara ya heshima, nidhamu na uadilifu wa taasisi za serikali. Mafunzo haya yanalenga kukuza ujuzi huo miongoni mwa watumishi,” alisema Dkt. Kimambo.
Mafunzo hayo yalihitimishwa na Dkt. Anita Lugimbana, Naibu Mkurugenzi wa Taaluma, Tafiti na Ushauri wa Kitaalamu, ambaye aliwataka washiriki kutumia ujuzi walioupata kuboresha huduma kwa umma na kuimarisha mahusiano ya kikazi ndani na nje ya nchi.
Sambamba na hilo Dkt. Anita aliwatunuku vyeti washiriki kutoka OTM kwa kwa kushiriki vyema mafunzo hayo.