Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

“TATHMINI SAHIHI YA WATUMISHI MSINGI WA UFANISI OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA ” - DPP Mwakitalu
15 Jan, 2026
“TATHMINI SAHIHI  YA WATUMISHI MSINGI WA UFANISI OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA ” - DPP Mwakitalu

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesisitiza umuhimu wa kufanya tathmini ya kina na halisi ya mahitaji ya watumishi ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa rasilimali watu katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha tathmini ya mahitaji ya Rasilimali Watu DPP Mwakitalu amesema kuwa Divisheni ya Rasilimali Watu ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taasisi yoyote, kwani husaidia kutambua na kutatua changamoto za kiutendaji, ikiwemo uhaba wa watumishi.

Kikao hicho kimewakutanisha wajumbe wote wa Menejimenti, Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa, Maafisa viungo wa Divisheni pamoja na  Vitengo kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

DPP Mwakitalu amesema kikao hicho ni dira na mwanga wa mwelekeo wa mahitaji halisi ya watumishi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, hatua itakayowezesha kuboreshwa kwa utoaji wa huduma za mashtaka kwa wananchi, hususan wale wanaoishi maeneo ya pembezoni.

Mwakitalu ameongeza kuwa kwa sasa huduma za mashtaka zinaendelea kusogezwa karibu zaidi na wananchi, hali inayoongeza mahitaji ya watumishi, huku akisisitiza umuhimu wa kila Divisheni kufanya tathmini sahihi ya mahitaji yake ili kuongeza ufanisi wa kazi na kuweka msingi imara wa maendeleo endelevu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Katika hatua nyingine, DPP Mwakitalu amewataka washiriki wa kikao hicho kushiriki kikamilifu na kwa umakini ili kufanikisha upatikanaji wa matokeo chanya na kubaini mahitaji halisi ya ofisi hiyo.

Aidha, ameeleza kuwa kukamilika kwa kikao hicho kutatoa taswira kamili ya mahitaji ya watumishi, na kwamba pale ambapo kutabainika uwepo wa uhitaji wa dhati, mamlaka husika zitaarifiwa ili ofisi iweze kupatiwa watumishi wenye uwezo, uadilifu na juhudi katika utendaji kazi.

Kikao hicho cha siku mbili kimeanza rasmi leo, Desemba 21, 2025, jijini Mwanza, kikilenga kutafuta suluhisho la changamoto ya upungufu wa watumishi katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.