Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

​RAIS MAGUFULI AMPONGEZA DPP NA TIMU YAKE
01 Oct, 2019
​RAIS MAGUFULI AMPONGEZA DPP NA TIMU YAKE

RAIS MAGUFULI AMPONGEZA DPP NA TIMU YAKE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza DPP Mganga na timu yake kwa kazi nzuri waliyofanya katika utekelezaji wa ushauri huo na pia kwa namna wanavyoiwakilisha vizuri Serikali katika kesi mbalimbali Mahakamani.

Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo tarehe 30 Septemba, 2019 alipopokea taarifa ya utekelezaji wa ushauri alioutoa tarehe 22 Septemba, 2019 kuhusu kuwasamehe washtakiwa wa makosa ya uhujumu walio tayari kukiri makosa yao, kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali.

Akipokea Taarifa hiyo ya DPP Mganga. Mhe. Rais Magufuli Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na mwitikio wa washtakiwa wengi kujitokeza kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali wanazodaiwa kuhujumu, na ameagiza washtakiwa wote waliofanya hivyo waanze kuachiwa kutoka Magerezani waliokokuwa wanashikiliwa.

Mhe. Rais amekubali ombi la kuongeza siku saba zaidi kwa DPP ili aendelee kupokea barua za washtakiwa ambao wapo tayari kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali na ameonya kuwa baada ya muda huo hakutakuwa na msamaha mwingine na kwamba kutolewa kwa msamaha huo hakuna maana kuwa makosa ya uhujumu uchumi yamefutwa.

“Nafahamu wapo wengine wanadanganywa na Mawakili wao kuwa wakikubali ndio watakuwa wamejifunga, hapana, wakisamehewa wamesamehewa, lakini sio lazima kuomba msamaha wakitaka kuendelea kubaki Magerezani ni shauri yao, lakini wale ambao wameomba msamaha na wamelipa waachieni hata leo, na wasirudie tena kufanya makosa hayo” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais amezitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Magereza na Jeshi la Polisi kuendelea kushirikiana na Ofisi ya DPP katika utekelezaji wa zoezi hilo.

Mhe. Rais amebainisha kuwa fedha zitakazokusanywa kutoka kwa washtakiwa hao zitalinufaisha Taifa kwa kwenda kutumika katika maendeleo ya wananchi ikiwemo ujenzi wa hospitali na barabara na kwamba ni matarajio yake kuwa washtakiwa watakaoachiwa watakwenda kushiriki ujenzi wa Taifa kwa njia zilizo halali.