NPS YASHIRIKI WAKILI MARATHON 2026 JIJINI DODOMA
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Makao Makuu pamoja na mikoa mbalimbali imeshiriki katika mbio za Wakili Marathon msimu wa kwanza 2026 zilizoandaliwa na Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania na kufanyika katika Viwanja vya Jamhuri, Jijini Dodoma.
Marathon hiyo imefanyika tarehe 31 Mei, 2026 na kuzinduliwa rasmi na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Zainabu Katimba, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Katimba alisema kuwa ushiriki katika mbio za marathon una manufaa makubwa kwa washiriki, ikiwemo kuimarisha afya na ustawi wa mwili, kuimarisha mshikamano na ushirikiano miongoni mwa mawakili, kukuza mahusiano ya kitaaluma, pamoja na kuzitangaza vyema taasisi za umma mbele ya wadau wa sekta ya sheria na wananchi kwa ujumla.
“Leo tumetekeleza kwa vitendo maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita yanayohamasisha wananchi kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Aidha, tumetoa mchango wetu katika kuunga mkono Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayolenga kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa huduma za kisheria,” alisema Mhe. Katimba.
Mbali na mashindano ya mbio za kilomita 5, 10 na 21, marathon hiyo pia ilitumika kama jukwaa la kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi, hatua inayodhihirisha dhamira ya wadau wa sekta ya sheria katika kuimarisha upatikanaji wa haki na huduma za kisheria nchini.
Ushiriki wa NPS katika Wakili Marathon 2026 unaakisi jitihada za taasisi hiyo katika kuhamasisha afya bora kwa watumishi, kuimarisha mshikamano kazini na kuunga mkono shughuli mbalimbali za kijamii zinazolenga kuleta maendeleo na ustawi wa jamii.
