Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

DPP AZINDUA KAMPENI YA NPS URITHI WA KIJANI
07 Jul, 2026
DPP AZINDUA KAMPENI YA NPS URITHI WA KIJANI

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amezindua  Kampeni ya “NPS Urithi wa Kijani” inayolenga kuimarisha utunzaji wa mazingira kupitia upandaji na utunzaji wa miti katika ofisi zote za NPS nchini ili kulinda mustakabali wa Taifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Julai 06, 2026 Jijini Dodoma  Bw. Mwakitalu amesema NPS itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kutunza mazingira kwa kutekeleza kikamilifu sera, miongozo na maelekezo ya Serikali kuhusu uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kuwa, pamoja na jukumu la msingi la NPS la kutoa huduma bora za mashtaka kwa wananchi, taasisi hiyo pia ina wajibu wa kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa vitendo ili kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.

"NPS imeanza kuwa ya kijani hata kabla hatujazindua kampeni hii ya mazingira. Hii inaonesha dhamira yetu ya dhati ya kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa na kulindwa wakati wote.” Amesema Mkurugenzi Mwakitalu

Pia amesema kuanzia siku ya uzinduzi huo, NPS itatekeleza kampeni hiyo kwa kaulimbiu isemayo "Pamoja Tunapanda Miti, Pamoja Tunalinda Mustakabali wa Taifa" ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha watumishi kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingiria huku akisisitiza kuwa mazingira ndiyo msingi wa uhai wa binadamu na viumbe wengine wote.

Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Mazingira ya NPS, Bi. Lucy Uwiso, amesema uzinduzi wa Kampeni ya NPS Urithi wa Kijani umeongeza nguvu katika juhudi za taasisi za kuhifadhi mazingira na kuhamasisha upandaji miti. Akieleza kuwa jumla ya miti 325 ilikuwa tayari imepandwa katika eneo la Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, huku miti mingine 90 ikipandwa wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.