NPS YAENDEDHA MAFUNZO KUHUSU MAJUKUMU YA KAMATI YA UKAGUZI
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) imeendesha mafunzo ya kujengeana uwezo kwa Kamati ya Ukaguzi, Menejimenti ya NPS na Kamati ya Ufuatiliaji na Utekelezaji wa hoja kwa lengo la kuimarisha uelewa wa pamoja kuhusu majukumu, wajibu na mipaka ya kila upande katika kusimamia na kutekeleza shughuli za taasisi.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 24 Juni, 2026 Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kila mshiriki anatambua wajibu wake ili kurahisisha utendaji kazi, kuongeza tija na kuimarisha uzingatiaji wa sheria, kanuni, miongozo na taratibu za Serikali.
Alieleza kuwa Menejimenti ndiyo inayobeba jukumu kubwa la kusimamia na kutekeleza shughuli za kila siku za taasisi, huku Kamati ya Ukaguzi ikiwa na wajibu wa kufuatilia na kuhakikisha majukumu hayo yanatekelezwa kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa ili kulinda rasilimali za umma na kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.
Aidha, Bi. Kileo alisisitiza kuwa Kamati ya Ukaguzi ni chombo muhimu katika kuimarisha uwajibikaji ndani ya taasisi kwa kuwa hufanya kazi kama jicho linalotathmini utekelezaji wa majukumu ya Menejimenti na kutoa ushauri wa kuboresha utendaji kazi. Aliwataka washiriki kuyatumia mafunzo hayo kujifunza namna bora ya kushughulikia na kujibu hoja za ukaguzi ili kuepusha kujirudia kwa hoja hizo na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kujenga uelewa wa pamoja kuhusu majukumu na mipaka ya Kamati ya Ukaguzi na Menejimenti, kuimarisha ushirikiano baina ya pande hizo na kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma kwa manufaa ya Taifa.
