NPS NGUZO MUHIMU YA UTAWALA WA SHERIA.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bw.Eliakim Maswi, amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni nguzo muhimu katika kusimamia utawala wa sheria nchini, kwa kuhakikisha kuwa sheria hazibaki kwenye vitabu pekee bali zinatekelezwa kwa vitendo katika maisha halisi ya wananchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, uliofanyika 18, Desemba, 2025 Jijini Mwanza, Bw. Maswi amesema kazi kubwa inayofanywa na ofisi hiyo imekuwa mwanga na msingi wa kuhakikisha ustawi, haki na usawa kwa jamii vinafikiwa.
Sambamba na hayo Bw. Maswi ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa juhudi zake za kuhakikisha masuala ya kisheria na mashauri yanasimamiwa na kuendeshwa kwa haki, uwazi na usawa, hali inayochangia kuimarika kwa ustawi wa taifa.
“Napongeza kwa kuimarishwa kwa mfumo wa maadili wa waendesha mashtaka ambao umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yanayoonekana hadi sasa ikiwemo uendeshaji wa mashuri kwa haraka, kupungua kwa msongamano wa Mahabusi Magerezani na kwa jinsi mnavyo endelea kusogeza huduma za kimashtaka karibu na wananchi kwa kufungua ofisi katika ngazi ya Wilaya.’’ Amesema Maswi
Awali, akitoa taarifa ya utendaji wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu, amesema ofisi hiyo imefanikiwa kupata ushindi wa asilimia 74 katika mashauri yanayosikilizwa katika mahakama za chini, huku idadi ya mashauri yanayoendelea katika Mahakama Kuu ikiendelea kupungua kwa kiwango kikubwa.
DPP Mwakitalu ameongeza kuwa ofisi inaendelea kuimarisha mkakati wa kuwafikia wananchi moja kwa moja, kwa lengo la kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na huduma za kisheria zinawafikia wananchi karibu na maeneo wanayoishi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Ramadhan Kingai,amesema ushirikiano mzuri uliopo kati ya Ofisi ya NPS na Jeshi la Polisi umeendelea kuwa chachu ya mafanikio katika kupambana na makosa ya jinai nchini.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kamishna wa sheria wa DCEA, Veronica Matikila amesema uwepo wa Mfumo wa Mashtaka wa Taifa (NPS) umefanikisha kutaifishwa kwa mali zilizopatikana kutokana na uhalifu wa dawa za kulevya.
Mkutano huo ni wa kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mwaka 2018, ukiwakutanisha watumishi wake wote kutoka mikoa mbalimbali nchini.