Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

NPS INA MCHANGO MKUBWA KATIKA KULINDA MASLAHI YA TAIFA - MTANDA
15 Jan, 2026
NPS INA MCHANGO MKUBWA KATIKA KULINDA MASLAHI YA TAIFA - MTANDA

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Said Mtanda, amesema kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) ina mchango mkubwa katika kulinda maslahi ya Taifa, kudumisha amani na kuhakikisha sheria zinasimamiwa na kufuatwa ipasavyo.

Bw. Mtanda ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Bonanza la watumishi wa NPS, lilofanyika  katika uwanja wa mpira wa CCM Kirumba, 20, Desemba, 2025 jijini Mwanza ambapo amesisitiza kuwa hakuna maendeleo bila kuwepo kwa amani na haki.

Mtanda ameeleza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha watumishi wa umma wanakuwa na afya njema, ndiyo maana imekuwa ikihimiza mazoezi ya viungo kwa vitendo ili kulinda afya zao wakati wote wa utumishi huku akiipongeza Menejimenti ya NPS kwa kutekeleza agizo hilo kwa vitendo kupitia bonanza hilo ambalo lilijumisha michezo mbalimbali.

Hata hivyo, RC. Mtanda amewakumbusha watumishi kuendelea kujali na kulinda afya zao, akisisitiza kuwa familia, jamii na Taifa kwa ujumla vinawategemea katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya jamii.

Awali, akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu, amepongeza uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa kuhakikisha usalama wa watumishi wa NPS wakati wote wa uwepo wao jijini Mwanza.

Bw. Mwakitalu amesema kuwa lengo la kuandaa michezo hiyo ni kuhakikisha watumishi wanakuwa na afya njema muda wote, pamoja na kuimarisha ushirikiano na mshikamano miongoni mwao ili kufanikisha dhima kubwa ya ofisi ya Kutoa huduma bora za mashtaka kwa wakati na usawa kwa wote.

Kwa upande wao, manahodha wa timu mbalimbali, akiwemo Bw. Simon Ntobi wa timu ya Menejimenti na Bw. Valence Mayenga, Nahodha wa timu ya Wakuu wa Mashtaka, wamesema kuwa michezo ni chanzo cha furaha na wamejitokeza kushiriki ili kuimarisha afya na kukuza mshikamano.

Naye Basilius Namkambe, mratibu wa bonanza hilo, amesema kuwa bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, pete, netiboli, voliboli, kuvuta kamba pamoja na michezo mingine.