NAIBU DPP AHIMIZA USHIRIKIANO KATIKA KUDHIBITI UHALIFU WA KIFEDHA
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Bibiana Kileo, amewataka Waendesha Mashtaka, Wachunguzi na Wapelelezi kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi zao kwa kufanya uchunguzi sambamba wa kifedha na kutumia ipasavyo ujuzi wanaoupata kama nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kifedha, hususan makosa ya utakatishaji fedha, ufadhili wa ugaidi na uhalifu wa kupangwa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha kuhusu matumizi ya taarifa fiche za kifedha katika kufanya uchunguzi sambamba wa kifedha, iliyofanyika tarehe 8 Mei, 2026 mkoani Pwani, Bi. Kileo amesema tathmini mbalimbali za kimataifa zilizopita zilionesha kuwepo kwa mapungufu katika mifumo ya kushughulikia uhalifu wa kifedha nchini licha ya uwepo wa sheria madhubuti.
Bi. Kileo amesema ushirikiano uliopo kati ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), TAKUKURU na Jeshi la Polisi unalenga kuziba mapengo hayo pamoja na kuimarisha kasi ya kushughulikia makosa ya utakatishaji fedha. Amefafanua kuwa tathmini hizo pia zilionesha udhaifu katika kudhibiti usafirishaji haramu wa fedha na ufadhili wa ugaidi, hali iliyochochea kuanzishwa kwa Kituo Jumuishi cha Kushughulikia Uhalifu wa Kifedha ambacho kimesaidia kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu huo.
Aidha, amesema mafunzo mbalimbali yanayoendelea kutolewa yamechangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha uwezo wa kudhibiti uhalifu wa kifedha nchini, huku akizitaka taasisi hizo kuendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Divisheni ya Makosa ya Udanganyifu, Utakatishaji Fedha na Rushwa, Bw. Christopher Msigwa, amesema warsha hiyo inalenga kuongeza uelewa na kuimarisha mifumo ya uchunguzi katika nyanja za kifedha.
Warsha hiyo imewakutanisha maafisa kutoka taasisi mbalimbali zilizopo katika mfumo wa haki jinai zikiwemo ; TAKUKURU, NPS, PCCB, Jeshi la Polisi, TAWA, TPA, TRA na DCEA.
