NAIBU DPP AHIMIZA MAPAMBANO DHIDI YA UHALIFU WA KIFEDHA
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amesema kuwa kutokana na ukuaji wa teknolojia duniani na ongezeko la uhalifu unaolenga kujipatia fedha kwa njia haramu, ni muhimu kuweka mifumo imara ya kudhibiti uhalifu wa kifedha ili kulinda na kujenga uchumi wa nchi.
Bi. Kileo ameyasema hayo wakati akifungua warsha ya siku mbili kuhusu matumizi ya taarifa fiche za kifedha katika kufanya uchunguzi sambamba wa kifedha inayofanyika tarehe 16 na 17 Juni, 2026 jijini Mwanza ikihusisha washiriki kutoka NPS, TAKUKURU na Jeshi la Polisi kwa upande wa Kanda ya Ziwa.
Amesema Kituo Jumuishi cha Kushughulikia Uhalifu wa Kifedha (ECC) kimekuwa kikifanya kazi kubwa kwa kushirikiana na vyombo vya uchunguzi na Upelelezi pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, hali inayochangia nchi kupata mafanikio mbalimbali katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kifedha, ikiwemo nchi kutoka kwenye uangalizi maalum wa kimataifa unaohusiana na masuala hayo.
“Kile tunachokifanya ni kikubwa sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Tunapaswa kutumia warsha hii kuifahamu vizuri ECC, kuelewa majukumu yake na kubadilishana uzoefu utakaotusaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu.” Amesema Naibu DPP
Aidha, amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 imeweka msisitizo katika kujenga uchumi imara, jambo linalozipa taasisi za haki jinai na taasisi za kifedha ikiwemo Kitengo cha Ujasusi wa Kifedha (Financial Intelligence Unit - FIU) wajibu mkubwa wa kulinda uchumi wa taifa dhidi ya athari za uhalifu wa kifedha.
Bi. Kileo aliongeza kuwa sambamba na kuanzishwa kwa ECC, viongozi wa taasisi za haki jinai walihakikisha wachunguzi, wapelelezi na waendesha mashtaka wanaopangwa kituoni hapo wanapatiwa mafunzo ya kutosha ya kitaalamu ili kuongeza ufanisi katika uchunguzi, upelelezi na uendeshaji wa mashauri yanayohusu uhalifu wa kifedha.
Pia amesema warsha hiyo itatoa fursa kwa washiriki kujifunza kwa vitendo mbinu mbalimbali za kukabiliana na uhalifu wa kifedha pamoja na kubadilishana uzoefu utakaosaidia kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu huo nchini.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Mfumo Endelevu wa Kupambana na Rushwa (BSAAT), Dkt. Boniventure Baya, ametoa pongezi kwa ECC kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na uhalifu wa kifedha.
Amesema kituo hicho kimechangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha wachunguzi wenye weledi na utaalamu wa hali ya juu katika uchunguzi wa makosa ya kifedha, jambo ambalo limeimarisha mifumo ya haki jinai na kuongeza imani ya wawekezaji nchini.
