Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

Mkurugenzi wa Mashtaka atembelea kambi ya wachezaji wa Mashtaka Sports Club Jijini Mwanza
14 Sep, 2025
Mkurugenzi wa Mashtaka atembelea kambi ya wachezaji wa Mashtaka Sports Club Jijini Mwanza

Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester Mwakitalu, ametembelea kambi ya wanamichezo wa Mashtaka Sports Club  wanaoshiriki mashindano ya SHIMIWI 2025 yanayoendelea Jijini Mwanza.

Ziara hiyo imefanyika tarehe 6 Septemba, 2025 katika eneo la Bwiru, Manispaa ya Ilemela, ambapo Bw. Mwakitalu alipata nafasi ya kuzungumza na viongozi pamoja na wachezaji wa timu hiyo, kwa lengo la kuwapa motisha kuelekea mashindano yaliyopo mbele yao.

Akizungumza na wachezaji, Mkurugenzi Mwakitalu alieleza kuwa michezo ni njia muhimu ya kuimarisha afya, mshikamano kazini, na mahusiano kati ya watumishi wa umma kutoka taasisi mbalimbali. Alisisitiza kuwa wachezaji hao wanapokuwa uwanjani hawawakilishi tu Ofisi ya Taifa ya Mashtaka bali pia wanabeba taswira nzima ya taasisi hiyo mbele ya jamii na taasisi nyingine za Serikali.

"Ni muhimu kudumisha nidhamu, heshima, ushirikiano, na kuzingatia uchezaji wa haki wakati wote wa mashindano." Aliongeza Bw. Mwakitalu. Pia aliwakumbusha wanamichezo hao kuzingatia maadili ya utumishi wa umma hata wanapokuwa kwenye mashindano, akiwataka kujiepusha na mienendo inayoweza kuchafua jina la Ofisi.

“Mnayo nafasi ya kuibeba na kuitangaza vyema taasisi yetu kupitia mashindano haya. Ushindi wenu si tu wa timu bali ni mafanikio kwa taasisi nzima,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka wanamichezo hao kuongeza bidii na kujituma ili kufikia hatua ya fainali na hatimaye kuchukua kombe la ushindi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mashtaka Sports Club, Bw. Juma Mahona, akizungumza kwa niaba ya wachezaji, alimshukuru Mkurugenzi wa Mashtaka pamoja na Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kuendelea kutoa nafasi na kipaumbele kwa ushiriki wa timu yao katika michezo ya SHIMIWI. Alieleza kuwa timu yao ipo imara na imejiandaa kikamilifu kukabiliana na wapinzani katika hatua mbalimbali za mashindano.

Bw. Mahona pia alieleza kuwa Mashtaka Sports Club imekuwa ikishiriki mashindano haya kwa miaka mitatu mfululizo, na kila mwaka timu hiyo imekuwa ikionyesha maendeleo makubwa – jambo linaloonesha dhamira ya dhati ya Ofisi ya kuwekeza katika afya na ustawi wa Rasilimaliwatu wake.

Mkurugenzi wa Mashtaka yupo Jijini Mwanza kwa ajili ya kushiriki hafla ya ufunguzi rasmi wa michezo ya SHIMIWI inayotarajiwa kufanyika tarehe 7 Septemba, 2025 katika viwanja vya CCM Kilumba, ambapo mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko.

Mashindano ya SHIMIWI 2025 yameanza rasmi tarehe 1 Septemba na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 16 Septemba, 2025. Mashtaka Sports Club inashiriki michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuvuta kamba, baiskeli, karata, bao, darts, mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, kurusha tufe na mingineyo.