MAFUNZO YA UHALIFU WA KIFEDHA KUONGEZA UWEZO KWA MAWAKILI WA SERIKALI
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) imeendelea kuimarisha uwezo wa mawakili wa Serikali katika kushughulikia mashauri ya uhujumu uchumi, udanganyifu na uhalifu wa kifedha kupitia mafunzo maalum yanayolenga kuwajengea washiriki uelewa wa kina kuhusu mbinu za kisasa za uchunguzi na uendeshaji wa mashauri hayo.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya Uratibu na Uendeshaji wa Mashauri ya Uhujumu Uchumi na yale yanayohusisha Uhalifu wa Kifedha Mei 29,2026 Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Kileo amesema mafunzo hayo yatawasaidia mawakili wa Serikali kwenda sambamba na mabadiliko ya aina za uhalifu unaotekelezwa kwa kutumia teknolojia na mbinu za kisasa za udanganyifu.
“Tunahitaji mawakili wetu wapate uelewa, wapate elimu namna ya kushughulika na mambo haya ya uhalifu wa kifedha. Hatuwezi kubaki nyuma wakati wahalifu wanaendelea kujifunza mbinu mpya kila siku,” amesema Bi. Kileo
Mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia Mei 26 hadi 29, 2026 katika ukumbi wa NPS Makao makuu, jijini Dodoma, yametolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Wataalamu wa Udhibiti wa Udanganyifu Tanzania (ACFE) na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka Mikoa 30 ya Kimashtaka pamoja na washiriki 33 kutoka NPS Makao Makuu.
Aidha, Bi. Kileo ameeleza kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia yamebadilisha namna makosa ya kifedha yanavyotekelezwa hivyo kuwepo kwa wataalamu wenye maarifa ya kisasa ni jambo muhimu katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati. Alisema mafunzo hayo yataongeza uwezo wa washiriki katika uchambuzi wa ushahidi pamoja na kufanya maamuzi sahihi ya mashtaka katika mashauri yanayohusisha uhalifu wa kifedha.
Pia Bi. Kileo amewataka washiriki kuhakikisha wanawafikishia wenzao maarifa waliyoyapata ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika vituo vyao vya kazi, na kuongeza kuwa NPS inaendelea kuweka mkazo katika kuwajengea uwezo mawakili wa Serikali ili waweze kukabiliana kwa ufanisi na changamoto mpya za uhalifu wa kifedha, udanganyifu na uhujumu uchumi.
