Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

KAIMU MKURUGENZI AWATAKA MAKATIBU SHERIA NA MAWAKILI KUZINGATIA WALIYOFUNDISHWA
09 Jan, 2022
KAIMU MKURUGENZI AWATAKA MAKATIBU SHERIA NA MAWAKILI KUZINGATIA WALIYOFUNDISHWA

Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ambae pia ni Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji wa Kesi Bi. Neema Mwanda amewataka Makatibu Sheria na Mawakili kuzingatia na kufanyia kazi yale yote waliyofundisha katika kipindi chote cha mafunzo kwani mfumo huu ulianzishwa kwa lengo la kusaidia kurahisisha shughuli zote za kiofisi.

"Ni jambo la faraja kuona kazi ya usanifu wa mfumo huu umekamilika, na jukumu lililopo mbele yetu sisi kwa sasa ni kuanza kuutumia mfumo huu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa"

Amezungumza hayo Mkurugenzi Mwanda wakati akihitimisha Mafunzo ya Utumiaji wa Mfumo wa Kielekitroniki wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika masuala ya Kesi kwa Makatibu Sheria na baadhi ya Mawakili wa Serikali wanaoshughulika na Takwimu yaliyoanza tarehe 5 Januari 2022 na kumalizika tarehe 8 Januari, 2022 Jijini Dar es salaam katika ofisi za TAGLA zilizopo Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

Aidha, alieleza kuwa licha ya changamoto zinazowakabili katika kuandaa taarifa za utekelezaji wa majukumu katika vituo husika vya kazi ambazo inabidi kutumia muda mwingi ili kuandaa taarifa hizo na wakati mwingine taarifa hizo zinakuwa sio sahihi. Ana imani kwamba kwa kupitia mfumo huo changamoto zote zitakwisha, na ufanisi utaongezeka na pia kusaidia katika masuala mbalimbali ya kimaamuzi na kimipango.

Kaimu Mkurugenzi alitoa wito kwa Makatibu Sheria na Mawakili kwenda kuwa mfano wa watumiaji bora na walimu wazuri wa mfumo huo kwa wengine kwa kuzingatia yale yote waliyofundishwa na wataalamu pamoja na kutekeleza kwa vitendo. Na endapo watakutana na changamoto yoyote ile au maboresho yanayohusiana na mfumo, basi wasisite kutoa taarifa kwa watu husika.

Aidha, Bi. Neema aliwashukuru Uongozi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa ushirikiano wao waliotuo katika kufanikisha suala zima la mafunzo ya mfumo huo wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.