Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

KAILIMA ATAKA KUTATULIWA KWA CHANGAMOTO YA UPELELEZI KUCHELEWA
10 Mar, 2022
KAILIMA ATAKA KUTATULIWA KWA CHANGAMOTO YA UPELELEZI KUCHELEWA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Ramadhani Kailima ameitaka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kushughulikia mambo muhimu sita ili kuboresha utendaji kazi na kutatua changamoto za uratibu wa Upelelezi.

Akizungumza katika hafla ya Ufunguzi wa mafunzo juu ya Makosa ya Mtandao, Uchunguzi na mbinu za Mashtaka Naibu Katibu Mkuu Kailima ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwataka Waendesha Mashtaka wa Serikali kutumia Mamlaka waliyopewa kisheria kutatua changamoto mbalimbali za kiutendaji.

Katika hotuba yake Bw. Kailima aliyataja mambo sita ambayo angependa yashughulikiwe.

Jambo la kwanza alilohitaji lishughulikiwe ni kuwepo kwa changamoto ya upelelezi kuchukua muda mrefu hivyo alitaka eneo hili lifanyiwe kazi kwa kuhakikisha upelelezi unaratibiwa vizuri na kwa haraka.

Eneo la pili Bw. Kailima aliomba Waendesha Mashtaka kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kutatua changamoto za ucheleweshaji mafaili.

Tatu alitaka Waendesha Mashtaka kukataa rushwa wanapotekeleza majukumu yao kwakuwa rushwa ni adui wa haki.

Nne aliwashauri kutimiza wajibu wao ipasavyo kwakuwa majukumu yao yanaakisi utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Mashtaka.

"Ukitembea, ukiongea, ukifanya kazi uonekane kama DPP kwakuwa huna namna ya kutenganisha majukumu yako na DPP". Alisema Naibu Katibu Mkuu Kailima.

Jambo la tano Naibu Katibu Mkuu Kailima alisisitiza umuhimu wa kuwa waadilifu kwa kuhakikisha kila jambo wanalolitenda kulifanya kwa uadilifu mkubwa.

Na jambo la sita aliwataka Waendesha Mashtaka kuendelea kutunza siri za Serikali.

Akimkaribisha mgeni rasmi kufuy mafunzo hayo Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu aliwataka Mawakili wa Serikali kuyatumia mafunzo hayo kikamilifu na kuboresha utendaji wao wa kazi.

Alisema ukuaji wa teknolojia huja na mambo mema lakini pia huambatana na changamoto hivyo mafunzo yaliyotolewa yatawaongezea weledi wa kupambana na uhalifu.

Bw. Mwakitalu alisema baadaye

Ofisi itawapima kutokana na utendaji wao wa kazi baada ya mafunzo.

Naye Wakili wa Serikali Mkuu Bi. Veronica Matikila alisema Makosa ya Mtandao yanaangukia katika Makosa ya kupangwa ambapo alieleza kuwa mafunzo wanayopatiwa Waendesha Mashtaka wa Serikali yanalenga kuwajengea ufahamu wa namna bora ya kuratibu upelelezi wa Makosa ya Mtandao na Makosa yanayoendana na hayo.

Naye Wakili wa Serikali Bi. Prosista Minja kutoka Songwe kwa niaba ya Washiriki wengine alimshukuru mgeni rasmi kwa kuwafungulia mafunzo na alishukuru Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kuwaandalia mafunzo ambapo aliahidi kwa niaba ya wenzake kuyatumia mafunzo kuboresha utendaji kazi.