JARIBIO LA UTEKAJI LAWAPELEKA JELA MIAKA SABA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kifungo cha miaka saba jela watuhumiwa wanne kati ya sita waliokuwa wakikabiliwa na kosa la jaribio la kumteka mfanyabiashara Deogratius Tarimo mkazi wa eneo la Kiluvya, jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa mwaka jana.
Hukumu hiyo imetolewa Oktoba 20, 2025 mbele ya Mheshimiwa Hakimu Mkazi Mwandamizi Ramadhani Rugemalira.
Katika kesi hiyo ya jinai Na. 34174/24, Fred Nsato na wenzake wanne walikuwa wanakabiliwa na kosa la jaribio la kumteka kinguvu mfanyabiashara huyo kwa lengo la kumjeruhi na kumlawiti lakini hawakufanikiwa baada ya mhanga kutumia vyema uimara wa umbo lake kubwa alipambana kujinusuru kwa kujizuia kuingia kwenye gari la watuhumiwa hao.
Kwa upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Daisy Makakala na Wakili wa Serikali Salma Jaffari, uliwasilisha mashahidi 15, akiwemo mhanga, mashuhuda wa macho, wataalamu wa ushahidi wa picha na video, Maofisa wa Polisi waliowakamata watuhumiwa, pamoja na mchunguzi wa kesi hiyo.
Baada ya kusikiliza ushahidi wote, Mahakama iliwakuta watuhumiwa wanne na hatia na kuwa hukumu kifungo cha miaka saba jela, huku watuhumiwa wawili wakiachiwa huru baada ya kubainika kuwa hakuna ushahidi wa kutosha uliowahusisha na tukio hilo.
Tukio hilo lililotokea tarehe Novemba 11, 2024 lilishuhudiwa na wananchi waliokuwepo eneo la tukio na kurekodiwa kwa video, ambayo baada ya muda mfupi ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kufuatia video hiyo watuhumiwa wanne walikamatwa Ifakara, mkoani Morogoro, walikokuwa wamejificha, huku wengine wawili wakikamatwa Jijini Dar es Salaam.