Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

JAJI MKUU APONGEZA TAASISI ZIUNDAZO UTATU KWA KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MAHABUSU MAGEREZANI
20 Aug, 2025
JAJI MKUU APONGEZA TAASISI ZIUNDAZO UTATU KWA KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MAHABUSU MAGEREZANI

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju apongeza taasisi zinazounda Utatu (Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, TAKUKURU na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya) kwa ushirikiano wao ambao umesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza msongamano wa Mahabusu magerezani.

“Niwashukuru Mkurugenzi wa Mashtaka pamoja na timu yako kwa hatua hii mliyoifanya ya kuanzisha Utatu huu kwani kupitia umoja huo umesaidia kutatua  changamoto mbalimbali tulizokuwa tunakumbana nazo magerezani ambazo kwa sasa zimepungua zikiwemo msongamano wa Mahabusu na wafungwa, ucheleweshwaji wa ukamilishwaji wa Upelelezi pamoja na ucheleweshwaji wa kusikilizwa kwa  kesi ambazo ndizo zilikuwa changamoto na kasoro za mfumo wa Haki Jinai katika Taifa letu"

Jaji Mkuu amebainisha hayo wakati akifungua Kikao kazi cha Menejimenti, Viongozi wa Mikoa na Wilaya wa Taasisi zinazounda Utatu kilichofanyika tarehe 19 Agosti, 2025 Jijini Dodoma.


Allifafanua kwa kusema
“Ukiangalia dira ya maendeleo ya mwaka 2050 imeweka kipaumbele kikubwa sana kwenye haki, mnavyofanya tathmini ya utendaji kazi wenu na kuweka mikakati mkumbukuke kuwa ninyi ni watu muhimu sana, lengo kuu la Serikali ni ustawi wa wananchi." 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema umoja na ushirikiano huo umewapa matokeo chanya kwa miaka  minne ambayo wamekuwa wakishirikiana na kuona mafanikio makubwa sana ikiwa ni pamoja na kuwa na ufanisi katika utendaji kazi wao ambao unaimarisha mifumo ya utoaji haki jinai nchini.

Aidha Mkurugenzi wa Mashtaka alitoa shukrani kwa taasisi binafsi ya PAMS Foundation kwa kuwa wadau muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu.

“Tunawashukuru wadau wote walioshiriki katika kikao kazi hiki na hii ni kwasababu ya umuhimu wa kikao hiki kwa kutambua kwamba wahalifu hawafungwi na mipaka lakini wanaweza kujificha na wakatenda uhalifu wao sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’’ Amesema Mkurugenzi Mwakitalu.

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Bw. Ramadhani Kingai amesema Kikao kazi hiki ni jukwaa muhimu la kuimarisha mshikamano katika taasisi zao katika mapambano dhidi ya uhalifu.

”Uhalifu una sura nyingi na haupambaniwi kwa jitahada za taasisi moja tunapaswa kushirikiana sio tu kati ya taasisi zetu nne zinazounda Utatu bali pia na wadau wengine wote wa mnyororo wa Haki Jinai kama vile Mahakama, Jeshi la Magereza, Jeshi la Uhifadhi, Uhamiaji na wadau wengine kwani ushirikiano huo ndio unaojenga uimara wa taifa letu katika kudhibiti uhalifu na kuhakikisha haki inatendeka.” Amesisitiza Mkurugenzi Kingai

Pia Mkurugenzi wa Oparesheni na Mafunzo kutoka Shirika lisilo la kiserikali PAMS Foundation Bw. Samson Kassala amesema umoja wao katika Haki Jinai ni sawa na viungo vya mwili ambavyo vinategemeana na kila kiungo kina sehemu ya kufanya kukamilisha mnyororo wote wa kuwasaidia  wananchi waweze kuwa salama