ECC KUENDELEA KUPAMBANA NA MAKOSA DHIDI YA UHALIFU WA KIFEDHA
Mkurugenzi wa Divisheni ya Makosa ya Udanganyifu, Utakatishaji Fedha na Rushwa, Bw. Christopher Msigwa, amesema kuwa Kituo Jumuishi cha Kushughulikia Uhalifu wa Kifedha (ECC) kitaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa kifedha kwa kuendeleza mifumo madhubuti itakayohakikisha Tanzania haigeuki kuwa kimbilio la wahalifu wa kifedha kujilimbikizia mali zisizo halali.
Bw. Msigwa ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu, mkoani Morogoro tarehe 26 Februari, 2026, kikilenga kuimarisha ushirikiano na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya ECC.
“Uwepo wa ECC inayoundwa na wadau waliopo katika mnyororo wa haki jinai umerahisisha kufanyika kwa upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya uhalifu wa kifedha kwa weledi na kwa wakati, hali inayochangia kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki,” amesema Bw. Msigwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo Jumuishi cha Kushughulikia Uhalifu wa Kifedha (ECC), Bw. Yamiko Mlekano, amesema kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kuwakutanisha wadau wanaounda ECC pamoja na taasisi mbalimbali zikiwemo taasisi za kifedha, mamlaka za udhibiti, taasisi za usimamizi wa masuala ya ardhi na bima.
Pia amefafanua kuwa kupitia kikao hicho, wadau wanapata fursa ya kujadili na kubadilishana uzoefu wa kikazi ili kuimarisha mikakati ya pamoja itakayowezesha mapambano dhidi ya uhalifu wa kifedha kuendelea kwa mafanikio makubwa na kuifanya Tanzania kuwa salama kiuchumi.
Aidha, Kituo Jumuishi cha Kushughulikia Uhalifu wa Kifedha (ECC) kinaundwa na taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU, Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Ofisi ya Rais, Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kupitia ushirikiano huo wa taasisi zilizo katika mnyororo wa haki jinai, ECC lina jukumu la kuratibu upelelezi na kuendesha mashtaka ya makosa ya uhalifu wa kifedha kwa ufanisi, weledi na kwa wakati, kwa lengo la kulinda uchumi wa Taifa.
