DPP MWAKITALU AZINDUA MWONGOZO JUU YA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWENYE MASUALA YA JINAI
Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amewaasa wananchi kuachana na vitendo vya kiuhalifu kwani uhalifu haulipi
Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema uwepo wa uhalifu uliokuwa ukizihangaisha baadhi ya nchi sasa limekuwa ni suala la kidunia kwakuwa uhalifu huo umekuwa ukizuia maendeleo ya jamii zetu.
Akizindua Mwongozo ya Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Masuala ya Jinai katika hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Bw. Mwakitalu alisema utoaji wa haki ikiwemo kuzuia vitendo vya uhalifu, ulinzi na Usalama wa raia ni msingi wa maendeleo ya jamii yoyote.
Mkurugenzi Mwakitalu alitaka uwepo wa ushirikiano wa nchi mbalimbali katika kupambana na uhalifu kwani juhudi za kupambana na uhalifu haziwezi kuishia katika nchi moja tu kwakuwa uhalifu wa kupangwa ni uhalifu unaovuka mipaka.
Mwakitalu aliendelea kueleza kuwa Tanzania imeridhia Mikataba mbalimbali ya Kimataifa ya kupambana na uhalifu wa kupangwa na unaovuka mipaka ikiwemo mikataba juu ya Ushirikiano wa Kimataifa ya kupambana na uhalifu.
Akizungumza katika hafla hiyo Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. David Concar alisema uzinduzi wa Mwongozo juu ya Ushirikiano wa Kimataifa juu ya kukabiliana na Jinai sio jambo dogo kwakuwa mamilioni ya watu duniani wanaathiriwa na kukua kwa Masuala ya uhalifu, kuongezeka kwa Masuala ya kigaidi na rushwa.
Balozi Concar alisema uzinduzi wa Mwongozo juu ya Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Masuala ya Jinai ni matokeo ya Ushirikiano katika ya ubalozi wa Uingereza na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kufanikisha juhudi mbalimbali za kupambana na uhalifu.
Naye Kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Balozi Manfred Kanti aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua iliyofikia kama chombo muhimu cha kupambana na uhalifu wa Kimataifa na ule unaovuka mipaka