Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

DPP ASISITIZA UTOAJI WA HUDUMA BORA KWA WANANCHI
01 Jul, 2026
DPP ASISITIZA UTOAJI WA HUDUMA BORA KWA WANANCHI

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu, amesisitiza umuhimu wa utoaji wa huduma bora kwa wateja kwa kuzingatia utu, usikivu na weledi ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na usawa. Amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) inahitaji watumishi wenye uwezo wa kuwahudumia wananchi wenye changamoto na mazingira tofauti, hususan katika masuala ya haki jinai, kwa uelewa, heshima na staha.

Bw. Mwakitalu amesema hayo Mei 29, 2026, wakati wa mafunzo ya mfumo wa kidijitali wa huduma kwa wateja kwa njia ya simu mara baada ya kutembelea Kituo cha Huduma kwa Wateja katika ofisi hiyo na kuzungumza na watoa huduma. Amesema mfumo huo unalenga kurahisisha utoaji wa huduma pamoja na kuongeza uwajibikaji kwa watumishi katika kuwahudumia wananchi.

“Uwepo wa mfumo huu utatuwezesha kupokea mrejesho wa huduma tunazozitoa kwa jamii, pamoja na kupokea malalamiko, maoni na ushauri kutoka kwa wananchi, jambo litakalorahisisha utoaji wa huduma hata bila wananchi kufika ofisini moja kwa moja,” amesema DPP Mwakitalu.

Aidha, DPP Mwakitalu amesema wateja wananaohitaji kupata huduma mara nyingi huwa wameathiriwa na vitendo vya kihalifu na kubeba maumivu mbalimbali, hivyo ni muhimu kwa watumishi kuzingatia namna ya kuwapokea na kuwahudumia kwa utu na weledi. 

Pamoja na hayo amewataka washiriki kuzingatia mafunzo yaliyotolewa ili kuuelewa mfumo huo pamoja na mbinu bora za kuwahudumia wateja kwa usikivu, uvumilivu na weledi ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za mashtaka kwa wakati na usawa. Mafunzo hayo ya siku 3 yametolewa na wataalamu kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao eGA