AFYA BORA NI MSINGI WA UTENDAJI BORA KWA WATUMISHI
Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) wametakiwa kulinda na afya zao kwani afya bora ni msingi wa utoaji wa huduma zenye ufanisi, hususani katika uendeshaji wa mashtaka.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu, leo tarehe 21 Desemba 2025, wakati akifungua semina ya siku moja kwa waelimishaji rika wa NPS, iliyowakutanisha waelimishaji kutoka AMikoa, Wilaya, Divisheni na Vitengo mbalimbali vya ofisi hiyo.
DPP Mwakitalu amesema kuwa NPS imekabidhiwa jukumu kubwa la kikatiba la kusimamia na kuendesha mashauri ya jinai katika mahakama zote nchini isipokuwa za kijeshi, hivyo utekelezaji wa jukumu hilo unahitaji watumishi wenye afya imara na bora ili kuongeza ufanisi wa kazi.
Katika hatua nyingine, DPP Mwakitalu amewataka watumishi waliopata dhamana ya kuwa waelimishaji rika kutumia nafasi hiyo ipasavyo kwa kuwaelimisha wenzao kuhusu namna ya kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwemo kuhamasisha udhibiti wa maambukizi ya VVU na UKIMWI mahali pa kazi.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Bibiana Kileo, amesema kuwa moja ya malengo makuu ya NPS ni kupambana na UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza ambayo hudhoofisha utendaji kazi.
Bi. Kileo amesema kuwa NPS inachukulia kwa uzito suala la afya kwa kuhakikisha elimu sahihi inawafikia watumishi wake katika maeneo yote nchini, ili wawe mabalozi bora wa elimu ya afya na kuwaelimisha wenzao kupitia mfumo wa waelimishaji rika.
Bi. Kileo ameeleza kuwa kutoa elimu hiyo kwa upana, watumishi watawezeshwa kuchukua hatua stahiki za kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, hatua itakayochangia kuboresha afya zao na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ndani ya taasisi.
Sambamba na hayo akizungumzia umuhimu wa semina hiyo kwa waelimishaji rika, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa NPS, Bw. Simon Ntobi, amesema kuwa ofisi hiyo imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za makusudi kuhakikisha mazingira rafiki na salama ya kufanyia kazi yanakuwepo kwa kuzingatia ustawi wa afya za watumishi wake.
