Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

WAZIRI MKUU ASISITIZA USHIRIKIANO WA KIKANDA NA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUPAMBANA NA UHALIFU
01 Jul, 2026
WAZIRI MKUU ASISITIZA USHIRIKIANO WA KIKANDA NA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUPAMBANA NA UHALIFU

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, amesema ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni nyenzo muhimu ya mafanikio katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa na uhalifu unaovuka mipaka na kupangwa.

Dkt. Mwigulu amesema hayo tarehe 4 Mei 2026 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 11 wa Umoja wa Waendesha Mashtaka Ukanda wa Afrika Mashariki, jijini Dar es Salaam, ambapo alisisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kupambana na uhalifu unaovuka mipaka na kupangwa.

Aidha, alieleza kuwa maendeleo ya teknolojia yameleta fursa pamoja na changamoto, ambapo baadhi ya wahalifu wamekuwa wakizitumia kufanya uhalifu kwa urahisi zaidi.

“Kama ambavyo uhalifu unaovuka mipaka na kupangwa unaongezeka bila kujali mipaka ya nchi, vivyo hivyo vyombo vya dola na mifumo ya haki ya jinai haviwezi kukabiliana nao kwa ufanisi bila kuwa na mifumo madhubuti ya ushirikiano wa kimataifa, hususan katika maeneo ya msaada wa kisheria na urejeshaji wa watuhumiwa,” amesema Dkt. Mwigulu

Aliongeza kuwa ipo haja ya nchi wanachama kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kubadilishana taarifa na kutumia teknolojia kwa ufanisi ili kukabiliana na uhalifu huo, hususan makosa dhidi ya wanyamapori.

Mkutano huo unajumuisha washiriki kutoka nchi 14 za ukanda wa Afrika Mashariki, unaofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 6 Mei 2026. Unatarajiwa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha mifumo ya haki jinai na kuongeza ufanisi wa waendesha mashtaka kwa kutumia teknolojia katika ukanda wa Afrika Mashariki.