Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA YAKABIDHI MSAADA KWA WATOTO WALIOPO KWENYE VIZUIZI VYA KISHERIA
07 Nov, 2022
OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA YAKABIDHI MSAADA KWA WATOTO WALIOPO KWENYE VIZUIZI VYA KISHERIA

Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania Bw. Sylvester Mwakitalu, amekabidhi msaada wa magodoro, taulo za kike, mashuka, mafuta na sabuni kwa Mkuu wa gereza la mahabusu Segerea Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hamisi Lissu.

Mkurugenzi Mwakitalu amesema msaada huo pamoja na vitu vingine umetolewa kwa ajili ya kuwahudumia watoto ambao wameshikiliwa kwenye vizuizi vya kisheria kutokana na makosa mbalimbali waliyoyafanya.

Msaada huo uliwasilishwa baada ya kuupokea kutoka Shirika la Utangazaji (TBC) ambalo lilitoa msaada huo kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ikiwa ni mchango wa Shirika hilo katika kuisaidia jamii.

" Nashukuru wadau wote wanaoendelea kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya uhalifu na leo asubuhi nimepokea msaada wa magodoro, mashuka, taulo za kike, sabuni na mafuta kutoka Menejimenti ya Shirika la Utangazaji Nchini( TBC) kwa ajili ya kuwapelekea watoto waliopo vizuizini na waliokinzana na sheria" anasema Mkurugenzi Mwakitalu

" Tunalo kundi kubwa la watoto ambao wanakaa kwenye Magereza na wazazi wao ( wanawake) ambao wanapatikana na hatia au wameshtakiwa kwa makosa ya jinai kwa sababu moja au nyingine anakosa dhamana na kwenda gerezani wakiwa na watoto wao na hawa ndio kundi kubwa ambalo lipo Katika Magereza yetu" anasema Mwakitalu.

Akimkabidhi msaada huo kwa DPP, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Moses Chitama, amesema msaada huo unalenga kurudisha fadhila kwa jamii, hivyo alitoa wito kwa jamii na wadau mbalimbili ikiwemo Sekta binafsi na mashirika ya Umma kuiga mfano kwa TBC wa kusaidia jamii.

Chitama amesema msaada huo wenye thamani ya Shilingi milioni tano (5,000,000/=) umetolewa na Shirika la Utangazaji Tanzania ( TBC) kwenda Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya kuupeleka gerezani kwa watoto wa wenye uhitaji maalumu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Segerea, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hamis Lissu, amesema msaada huo umekuja wakati muafaka kutokana na watoto kuhitaji misaada mbalimbali ikiwemo magodoro na sabuni na vitu vingine.

" Msaada huu utaenda kutumika kama ulivyokusudiwa kwa walengwa, hivyo tunaomba wadau wengine waige mfano kama huu ulioonyeshwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Shirika la Utangazaji nchini kwa kuwajali wahitaji" amesema SSP Lissu.