Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

NPS NI NGUZO MUHIMU KATIKA KUHAKIKISHA HAKI INATENDEKA NA MASLAHI YA UMMA YANALINDWA
01 Jul, 2026
NPS NI NGUZO MUHIMU KATIKA KUHAKIKISHA HAKI INATENDEKA NA MASLAHI YA UMMA YANALINDWA

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Zainab Katimba amesema  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) ni nguzo muhimu katika kuhakikisha haki inatendeka na maslahi ya umma yanalindwa kupitia mashauri ya jinai yanayosimamiwa na kuendeshwa ofisi hiyo, hivyo nafasi ya kuajiri watumishi wapya ni dhamana kubwa na yenye heshima katika kuboresha huduma za kimashtaka nchini.

Mhe. Katimba amesisitiza hayo wakati akifungua Mafunzo elekezi ya awali kwa waajiriwa wapya wa NPS yanayofanyika kuanzia tarehe 15 hadi 19 Aprili, 2026 Jijini Arusha ambapo alieleza kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwajengea uelewa mpana wa majukumu yao, miiko ya kazi, misingi ya sheria na utamadumi wa utumishi wa umma pia ni fursa ya kujenga mshikamano baina yao ili kuwawezesha kufanya kazi kwa ushirikiano bila kujali tofauti za kada.

”Tumieni nafasi hii adhimu kutumikia serikali kwa uadilifu, weledi, moyo wa kujitoa na kuhakikisha kwamba haki kwa wananchi mtakaowahudumia inapatikana.” Amesema Naibu Waziri

Mafunzo haya yanajumuisha washiriki 162 wa kada mbalimbali wakiwemo Mawakili wa Serikali, Makatibu Sheria, Madereva, Wahasibu, Wasaidizi wa Hesabu, Watakwimu, Afisa Tehama, Watunza Kumbukumbu, Waandishi Waendesha Ofisi  na Afisa Habari.

Pamoja na ongezeko hilo, uhitaji wa watumishi bado ni mkubwa kwani NPS inaendelea kusogeza huduma karibu na wananchi  katika wilaya zote nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati.

Mhe. Katimba amesema Serikali itaendelea  kuiwezesha NPS kwa kutoa mafunzo mbalimbali, vitendea kazi na kuboresha mazingira  ya kazi ili  kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Aidha, amewahimiza washiriki hao kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma na kuwa waadilifu wakati wote wa utekelezaji wa majukumu watakayopangiwa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema watumishi hao watakwenda kuongeza nguvu katika ofisi zilizokuwa na uhaba wa watumishi hususan ofisi za wilaya.