NAMTUMBO WAFIKIWA NA HUDUMA ZA MASHTAKA
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Homera amesema Serikali imetenga zaidi ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Namtumbo, huku ofisi hiyo ikiwa miongoni mwa wilaya 21 nchini zilizokabidhiwa magari mapya kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi na utoaji wa huduma za mashtaka kwa wananchi.
Dkt. Homera ameyasema hayo Mei 11, 2026 wakati wa hafla ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Wilaya ya Namtumbo pamoja na kukabidhi gari kwa ofisi hiyo, ambapo alieleza kuwa upatikanaji wa haki ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa kwani wananchi wanapopata haki kwa wakati huweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya kiuchumi.
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi za mashtaka katika mikoa yote 26 pamoja na kufungua zaidi ya ofisi 118 za wilaya nchini kote, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za mashtaka.
“Serikali imeamua kusogeza huduma hizi karibu na wananchi ili kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za haki. Kupitia juhudi hizi, wananchi wataendelea kupata huduma bora zaidi kwa wakati na usawa kwa wote” amesema Dkt. Homera.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Bw. Slyvester Mwakitalu amesema kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Namtumbo ilianzishwa rasmi mwezi Oktoba, 2025 ikiwa sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kusogeza huduma za mashtaka karibu na wananchi.
Ameongeza kuwa ujenzi wa jengo jipya na upatikanaji wa gari vitasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi pamoja na kurahisisha upatikanaji wa haki jinai kwa wananchi wa Wilaya ya Namtumbo.
