MAGARI 21 KUONGEZA KASI YA UTENDAJI NPS
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera, amezindua magari 21 yatakayosaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Ofisi za Mashtaka za Wilaya nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika tarehe 03 Mei, 2026 Jijini Dar es salaam, Mhe. Dkt. Homera amesema kuwa magari hayo ni nyenzo muhimu zitakazorahisisha utekelezaji wa majukumu ya kila siku, hususan katika uendeshaji wa mashauri ya jinai.
“Ni imani yangu kuwa upatikanaji wa vitendea kazi hivi utaongeza ufanisi na kasi ya utendaji wa kazi za mashtaka. Hivyo, ni wajibu wetu kufanya kazi kwa bidii, kwa ushirikiano, na kuhakikisha mashauri yote ya jinai yanakamilika kwa wakati,” amesema Mhe. Dkt. Homera.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka nane, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatua iliyochangia kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani pamoja na malalamiko kutoka kwa wananchi. Aidha, juhudi hizo zimepelekea kupungua kwa idadi ya mahabusi na wafungwa magerezani.
Vilevile, Waziri Homera amebainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatambua na kuthamini mchango wa NPS katika kuchochea maendeleo ya nchi hivyo upatikanaji wa magari hayo 21 ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha huduma za mashtaka zinawafikia wananchi kwa wakati.
Aidha, amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali inatarajia kununua magari mengine 30 kwa ajili ya Ofisi za Mashtaka za Wilaya 30 ambazo bado hazijapatiwa magari ili kuendelea kuboresha mazingira ya kazi na utoaji wa huduma.
Pia amewataka madereva watakaokabidhiwa kuendesha magari hayo kuyatunza na kuyatumia kwa uangalifu ili yaweze kudumu na kuleta tija iliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester Mwakitalu, amesema kuwa ujio wa magari hayo 21 utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya uhaba wa vitendea kazi katika ofisi za mashtaka za wilaya, hususan kwa zile zilizokuwa hazina magari.
