DPP AWAPONGEZA WATUMISHI KWA KUFANYA KAZI KWA BIDII
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Bw. Sylvester Mwakitalu amewapongeza watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kufanya kazi kwa bidii katika kipindi chote cha mwaka mmoja kuanzia Mei Mosi iliyopita hadi kufikia sasa, amesema yeye pamoja na timu ya Menejimenti wanathamini mchango mkubwa wa watumishi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi, huku akiwahimiza kuendelea kuongeza juhudi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
DPP Mwakitalu ametoa pongezi hizo alipokuwa akizungumza na watumishi wa ofisi hiyo katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Njombe, mara baada ya kushiriki Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa mkoani humo tarehe 01 Mei, 2026.
“Tunapoendelea kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi, tukumbuke kuwa tunabeba dhamana kubwa ya kuwawakilisha wananchi ambao hawawezi kujisimamia wenyewe mahakamani; hivyo tunapaswa kutekeleza wajibu huo kwa uadilifu na kuhakikisha haki inatendeka kwa niaba yao,” amesema DPP Mwakitalu.
Aidha, DPP amesisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha kesi zinazofunguliwa mahakamani zinamalizika kwa wakati, huku akiwahimiza watumishi kuendelea kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kuendesha mashtaka kwa weledi, uaminifu na uadilifu.
“Ninyi ndiyo nguzo ya haki jinai katika nchi hii; mkishindwa kutimiza wajibu wenu ipasavyo, kuna wananchi wataumia, watapoteza haki zao na wengine kutokutendewa haki,” ameongeza DPP Mwakitalu.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Bibiana Kileo, amewashukuru watumishi wote kwa ushirikiano wanaouonesha katika kuimarisha taswira ya taasisi, na kuwasisitiza kuendelea kuwa watiifu kwa miongozo na taratibu za kazi ili kufanikisha malengo ya Ofisi.
Naye Mkurugenzi wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bw. Simon Ntobbi, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza upendo kazini pamoja na mshikamano miongoni mwa watumishi, akibainisha kuwa hali hiyo huongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi.
