BARAZA LA WAFANYAKAZI NPS LAPITISHA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2026/2027
Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) limepitisha mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, huku watumishi wakihimizwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na uwajibikaji ili kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu.
Mkutano huo umefanyika tarehe14 Aprili, 2026 mkoani Arusha, ukihusisha wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kujadili utekelezaji wa mpango na bajeti pamoja na mwelekeo wa mwaka mpya wa fedha.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti aliwapongeza watumishi wa NPS kwa juhudi wanazoendelea kuonyesha katika utekelezaji wa majukumu yao, na pia alimpongeza Mkurugenzi wa Mipango pamoja na timu yake kwa maandalizi mazuri ya bajeti iliyopita na bajeti ya mwaka 2026/2027.
“Kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa bidii ili tuendelee kujenga hoja ya msingi ya kuongezewa rasilimali zaidi kama vile vitendea kazi vya kisasa, majengo pamoja na rasilimali watu kwa manufaa ya taasisi na wananchi jumla,” alisema Bw. Mwakitalu.
Aidha, Mwenyekiti alisisitiza kuwa rasilimali watu ni msingi muhimu wa mafanikio ya NPS, huku akiwataka watumishi kuzingatia nidhamu ya kazi, kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kujengeana uwezo ili kuendelea kutoa huduma bora za mashtaka, kwa wakati na usawa kwa wote.
