Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

"Uchunguzi wa Makosa ya kifedha ni nguzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kiuchumi". Mhe. Rose Ebrahim
26 Apr, 2025
"Uchunguzi wa Makosa ya kifedha ni nguzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya uhalifu  wa kiuchumi". Mhe. Rose Ebrahim

Jaji Mfawidhi wa Mahamaka Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Rose Ebrahim amesema uchunguzi wa Makosa ya kifedha ni nguzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya uhalifu huu wa kiuchumi kwani wahalifu wengi wa makosa hayo wamekuwa wakiibua mbinu mbalimbali za kidigitali ikiwemo kuunda mitandao tata isiyofikikaa kirahisi na mbinu za kawaida.

“Kwenye makosa ya kifedha wahalifu wengi huwa wanatumia mbinu za kiteknolojia kutenda au kuwezesha utendekaji wa makosa hayo, hivyo Wapelelezi na Waendesha Mashtaka lazima wawe na ujuzi wa kutosha kufaa kukusanya ushahidi wa kielektoniki na kufuata sheria zilizowekwa ili kusimama vyema bila kupoteza ushahidi”.

Mhe. Jaji ameyasema hayo wakati akifungua Mafunzo kwa wadau wa Haki Jinai kuhusiana na Uchunguzi wa Makosa ya Kifedha na Uchunguzi wa Kisayansi yanayofanyika tarehe 25 na 26 Aprili, 2025 Mkoani Morogoro.

Jaji Mfawidhi amesema ni muhimu  mafunzo hayo kufanyika kwa kila mamlaka ili kuweka utaratibu wa kuwa na mafunzo endelevu ya kubaini mbinu zinavyobadilika kila kukicha kwani itasaidia kupata nafasi ya kubadilishana uzoefu kwa mambo au mbinu na changamoto ambazo wengine wanakutana nazo na namna bora ya kukabiliana nazo.

Katika hatua nyingine Mhe. Jaji amesisitiza juu ya umuhimu mkubwa wa Ushahidi wa Kisayansi katika utendaji wa haki ambapo Sayansi na Teknolojia vimeshika atamu.

“Ni lazima tuwe na maarifa na mbinu za kutosha za kiupelelezi na ukusanyaji ushahidi unaojibu makosa ya kifedha ili kuisaidia mahakama kutoa maamuzi yaliyosahihi kwa upande wa mashtaka na kuweza kutaifisha mali zinazotokana na makosa husika.’’ Amefafanua Mhe. Jaji Rose.

Sambamba na hilo amewataka Waendesha Mashtaka na Wapelelezi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuwawezesha kupata ushahidi wa uhakika na uliokamilika.

Aidha, amesema Mashtaka bila ufuatiliaji wa mali ni ushahidi nusu, ambao bado haujakamilika. Uhalifu wa kifedha sio tu kuwafikisha wahusika mahakamani bali ni kuhusu Urejeshaji wa mali, uwajibikaji na kutoa fundisho kwa wengine.

Mali yoyote au fedha inayoporwa kutoka kwa umma au wananchi inapaswa kurejeshwa na kila mhalifu hanabudi ya  kuadhibiwa pamoja na kupokonywa faida ya uhalifu huo.

Pia amesema mafunzo hayo yakawe chachu kwao katika kupambana na uhalifu huo wa kifedha na kutumia ushahidi wa kisayansi ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote atakaethubutu kuchezea mali za taifa, kuzipora au kuzihujumu na kuachwa akafaidika kwa namna yoyote ile.


Kwa upande wake Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Morogoro Bi. Tarsila Gervas ameeleza lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea uwezo Wapelelezi na Waendesha Mashtaka katika masuala ya Makosa ya kifedha pamoja na makosa mengine yanayohusisha Ushahidi wa Kisayansi.

Pia amesema mafunzo hayo ni dhamira ya dhati kwa Mkoa wa Morogoro katika kuhakikisha wanafanya upelelezi na uendeshaji wa mashtaka ambao unakuwa na ufanisi mkubwa na unaolenga kukomesha uhalifu katika mkoa huo.

"Tunataka kuujenga mkoa salama ambapo wananchi wake wanaweza kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa amani pasipo kusumbuliwa wala kuwa uwoga wa vitendo vya kiuhalifu." Amefafanua Bi. Tarsila

Aidha mafunzo hayo yamehusisha taasisi mbalimbali zinazounda mnyororo wa haki jinai zikiwepo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU, TAWA, TANAPA, TFS, Jeshi la Polisi, na Uhamiaji.