Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

DPP AZINDUA MWONGOZO WA USHIRIKIANO WA WADAU KATIKA UPELELEZI WA UTAKATISHAJI FEDHA HARAMU, UGAIDI NA UFADHILI WA UGAIDI.
30 May, 2023
DPP AZINDUA MWONGOZO WA USHIRIKIANO WA WADAU KATIKA UPELELEZI WA UTAKATISHAJI FEDHA HARAMU, UGAIDI NA UFADHILI WA UGAIDI.

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amezindua Mwongozo wa Ushirikiano wa Wadau katika Upelelezi wa Utakatishaji  Fedha Haramu, Ugaidi na Ufadhili wa Ugaidi kwa lengo la kudhibiti na kupambana na makosa hayo.

Uzinduzi huo umefanyika tarehe 24 Mei, 2023 Jijini Dodoma, ambapo katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mwakitalu ameeleza kuwa Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yamewarahisishia wahalifu kufanya makosa mbalimbali bila kutambulika zaidi, hivyo kupitia Mwongozo huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti uhalifu huo.

"Leo Tumezindua Mwongozo wa namna ambavyo Taasisi zinazohusika na mapambano dhidi ya makosa hayo jinsi zitakavyoshirikiana na kuratibiwa vizuri kwa shuguli zote zinazohusiana na makosa ya uhalifu wa namna hiyo. Na ushirikiano ya Taasisi hizi ni zile Taasisi za Uchunguzi, Taasisi za Usimamizi wa Sheria na Taasisi zingine za kifedha." Amefafanua hayo Mkurugenzi Mwakitalu.

 Aidha, DPP ameeleza kuwa Mwongozo huo utaziongoza Taasisi hizi ambazo zitaratibiwa vizuri, na taarifa za uhalifu zitakazopatikana ni namna gani zitapelekwa kwenye chombo kingine ambacho chenye Mamlaka ya kuweza kuzishughulikia,  kuzichunguza na namna ambavyo zitafika kwenye hatua ya Mashtaka kama makosa hayo yatathibitika kwamba upo ushahidi wa kutosha wa kuyaendesha Mahakamani.

Mkurugenzi Mwakitalu amezisihi Taasisi kushirikiana kwa pamoja ili muhalifu anapofanya kosa asije akatoka bila kuguswa na mkono wa sheria.

"Makosa haya yapo na tunazo kesi nyingi Mahakamani ambazo zipo zinaendelea katika hatua mbalimbali na wapo watu ambao tunawashtaki kwa makosa ya Utakatishaji Fedha, lakini pia tunazo kesi za ugaidi zinaendelea katika hatua mbalimbali Mahakamani." Amesema Mwakitalu.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Bw. Aretas Lyimo amesema Madawa ya Kulevya ni eneo moja wapo ambalo linatumika sana katika utakatishaji Fedha na Ufadhili wa Ugaidi, hivyo Mwongozo huo utasaidia kuunganisha nguvu ya pamoja katika kupambana na Uhalifu hapa nchini.

"Mwongozo huu utatusaidia sana kupunguza makosa mbalimbali ya kiuhalifu hususani Makosa ya Kupangwa ambayo Taasisi zetu zinashirikiana katika kuyafanyia kazi."  Amefafanua Jenerali Lyimo.

Utakatishaji fedha, Ugaidi na Ufadhili wa Ugaidi ni maeneo ambayo Serikali inaenda kuyadhibiti ili Taifa liendelee kuwa salama kwa watu wake.