DPP AWATAKA WAAJIRIWA WAPYA KUFANYA KAZI KWA WELEDI
Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu ametoa wito kwa waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufanya kazi kwa Uadilifu na Weledi ili kuhakikisha Haki, Amani na Usalama vinapatikana nchini.
Mkurugenzi Mwakitalu ameyasema hayo wakati akitoa neno la utangulizi kwenye Mafunzo elekezi ya awali kwa waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yanayofanyika mjini Morogoro kuanzia tarehe 15 hadi 21 Aprili, 2023
Mafunzo hayo yanalenga katika kuwajengea uwezo watumishi waajiriwa wapya ili kuwawezesha kufahamu namna ya kuenenda na kufanya kazi kama watumishi wa Serikali.
Akizungumza katika mafunzo hayo Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba Mhe. Ayub Mwenda amewataka waajiriwa wapya kujibidiisha kwa Weledi na kimaadili katika kutekeleza majukumu ya kikatiba waliyopewa.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es salaam Mhe. Edwin Kakolaki aliwapongeza waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kuwataka kuepuka tamaa na kuridhika na watakachokuwa wanapata na kujenga uaminifu.