Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

DPP AWAELEKEZA WANAWAKE WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA KUTUNZA RASILIMALI ZA SERIKALI
11 Mar, 2025
DPP AWAELEKEZA WANAWAKE WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA KUTUNZA RASILIMALI ZA SERIKALI

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuwa mstari wa mbele kutunza rasilimali walizopewa na serikali ili kuendelea kuwasaidia katika majukumu yao ya kila siku.

“Muwe ni watu wa kujali na mtunze rasilimali kidogo ambazo tumezipata kwani Serikali imewekeza fedha na rasilimali zingine na tunatarajia wanawake mtakuwa kinara katika kutuvusha kwenye hili hivyo tunataka kuona matokea ya uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeufanya katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.’’ 

Mkurugenzi wa Mashtaka ameyasema hayo wakati aliposhiriki  chakula cha jioni pamoja na  watumishi wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutoka Makao Makuu Jijini Dodoma, Arusha, Mkoa wa Kilimanjaro na Manyara mara baada ya kushiriki kwenye kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yalifanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 8 Machi, 2025.

Mkurugenzi Mwakitalu amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ina watumishi wengi wa kike ambao ni zaidi ya asilimia 65 hivyo wanapaswa kujiamini ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kwa kujituma.

“Utendaji kazi wetu lazima uonyeshe kwamba taasisi yetu ina wanawake wengi kwasababu nyie ni watu wa kujali. Tunataka watu waone Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inafanya vizuri kwasababu ya wanawake.’’ Amefafanua hayo Mkurugenzi Mwakitalu

Pia Mkurugenzi Mwakitalu ametoa pongezi kwa wanawake hao kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika kipindi chote cha  Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wakati walipotembelea banda la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Jijini Arusha.  

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amewataka wanawake wa ofisi hiyo kuutumia uwezo mkubwa waliopewa na  Mwenyezi Mungu wa Ualimu,Ulezi  kuipendezesha na kuzidi kuiinua  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kazi zao kwa kuzingatia kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo inasema "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji.

‘Kama Kauli mbiu ya Mwaka huu 2025 inavyosema,Tuutumie uwezo mkubwa kabisa ambao Mungu ameweka ndani yetu ili kuhakikisha taasisi yetu inaongoza  kutenda haki ndani ya nchi hii hata watakapotafuta siri ya mafanikio ya Ofisi yetu watambue kwamba ni  sababu ya mchango mkubwa pia wa wanawake  waliopo ndani ya ofisi hiyo.” Amesema Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka

Aidha, amewataka wanawake hao kuhakikisha kuwa  wanapoondoka mahali hapo waondoke wakiwa na  chachu ya kufanya kazi kwa bidii,kuwafundisha na kulea wengine na kuahidi kutokuiangusha taasisi yao.

‘’ Ipo nguvu kubwa ndani ya mwanamke ya kuratibu mambo,kufundisha na kulea.
 Ninaomba iyo nguvu pia tuiweke kwenye taasisi yetu kuwafundisha  watumishi walio chinj yetu, ili tuweze kuleta matunda na kufikia maono makubwa ya taasisi yetu.’’ Amefafanua Naibu DPP