Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

DPP AKABIDHI MADINI, VITO NA FEDHA ZILIZOTOKANA NA KESI ZA UHUJUMU UCHUMI KWA KATIBU MKUU HAZINA
28 Aug, 2019
DPP AKABIDHI MADINI, VITO NA FEDHA ZILIZOTOKANA NA KESI ZA UHUJUMU UCHUMI KWA KATIBU MKUU HAZINA

DPP AKABIDHI MADINI, VITO NA FEDHA ZILIZOTOKANA NA KESI ZA UHUJUMU UCHUMI KWA KATIBU MKUU HAZINA

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Bw. Biswalo Mganga amekabidhi madini , vito na fedha za kigeni za nchi mbalimbali zenye thamani ya shilingi bilioni 3.126 zilizotokana na kesi za uhujumu uchumi kwa Katibu Mkuu Hazina Bw. Dotto James . Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Dar es salaam katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania. Akikabidhi madini, vito na fedha hizo DPP Biswalo amesema madini yaliyotaifishwa ni kilo 25.546 za dhahabu zenye thamani ya Dola za Marekani 913,954.72 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh.bilioni 2 ( 2,102,095,941.) Kilo 76,020.20 (Tani 76) za colored gemstones zenye thamani ya zaidi ya Dola milioni 2 (2,638,349.95) ambazo ni sawa na zaidi ya Sh. Bilioni 6

(6,068,204.885,) Tanzanite gramu 888 zenye thamani ya Dola 3,197 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh. Bilioni 7 (7,353,348 ambazo haijakabidhiwa siku ya leo) pamoja na fedha za kigeni za mataifa mbalimbali 15 zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 1 (1,023,608.515.12) .

Amesema mali na fedha hizo zilikuwa zimetunzwa sehemu mbalimbali wameamua kuzikabidhi kwa kwa Katibu Mkuu Hazina ambaye ndiye msimamizi wa mali za Serikali kwa mujibu wa sheria ili kuepuka uwezekano wa kupotea au kumbukumbu kupotea.

Akipokea mali hizo na fedha Katibu Mkuu Hazina Bw. Dotto James ameishukuru na kuipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanywa hadi kutaifishwa kwa vito, madini na fedha hizo na kuwaahidi Watanzania kuwa Serikali itazitumia fedha zitakazotokana na mali hizo kwa maendeleo ya Taifa na Watanzania kwa ujumla.

“Niko hapa leo hii kupokea mali hizi kwa niaba ya Watanzania na niwaahidi kuwa nazikabidhi hapa Benki Kuu kwa ajili ya kuzitunza na zitakuwa salama, nawashukuru na niwapongeze Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kazi nzuri na kubwa mliyoifanya hadi kuwezeha mali na fedha hizo kutaifishwa, niwaahidi kuwa mali na fedha hizo zitatumiwa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na watanzania wote kwa ujumla,” alisema Kaibu Mkuu James.

Awali akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhianoo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ameipongeza NPS na Mahakama kwa kuwezesha kutaifishwa na mali hizo na kuwataka kuendelea kuchapa kazi huku akiwaahidi kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono katika kuhakikisha kazi zao zinafanikiwa na hivyo kulinda maslahi ya Taifa.

Naye Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Phillip Mpango pia ameipongeza NPS na Mahakama kwa kuwezesha kupatikana kwa mali na fedha hizo na hivyo kudhihirisha kuwa Tanzania sio nchi masikini na inaweza kuendelea na kutoa huduma bora za afya , maji na elimu kwa wananchi wake bila ya kutegemea mikopo ya yenye masharti magumu.

Amemuomba Waziri wa Katiba na Sheria kuwaombea vyeti vya utambuzi kwa Mkuu wa Utumishi wa umma nchni ili kutambua kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na watumishi waliowezesha kupatikana kwa madini na fedha hizo huku akimuagiza Katibu Mkuu Hazina kuangalia namna ya kuwapatia kifuta jasho watumishi husika ili kutambua mchango wao kwa taifa .

Naye Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko akizungumza katika hafla hiyo amewataka watu wanaojishughulisha na shughuli za maadini isivyo halali kutambua kuwa muda wa kufanya hivyo haupo tena na Serikali itapambana nao kwa maslahi ya Taifa.

“Niwaambie wote wanaojishughulisha na biashara ya madini bila kibali kuwa zama hizi sio zao tena , na hawatapata nafasi za kuiibia tena nchi hii, tutapambana nao kwa nguvu zote na ndio maana leo hii mnaona tukikabidhiwa mali hizi, hii ni ishara kuwa tuko macho na tutapambana na yeyote yule anaetaka kutuibia” alisema mhe. Biteko.

Madini, vito na fedha hizo zimetokana na kesi za uhujumu uchumi ambazo ofisi ya Taifa ya Mashtaka iliziendesha na kumalizika kati ya mwaka 2017 na 2018 jijini Dar es Salaam ambapo washtakiwa waliokuwa wakikabiliwa na kesi hizo walitiwa hatiani na Mahakama iliamuru kulipa faini au kutumikia kifungo gerezani na kutaifisha maadini, vito na fedha walizokutwa nazo walipokuwa wakisfirisha madini hayo bila ya kuwa na kibali.